2016-02-19 15:41:00

Falsafa ya Samaki ni kukesha!


Watu wengi hufuatilia kwa karibu sana kipindi cha mahojiano katika vyombo vya habari. Wasikilizaji hutafakari na kujifunza busara ya mwuliza maswali na hekima ya anayejibu. Dominika iliyopita tuliiona jeuri ya shetani akimhoji Yesu maswali kwa ujanja, na jinsi Yesu alivyoyapangua kwa hekima hadi shetani mwenyewe akafyata mkia na “kumwacha Yesu kwa muda.”(Lk 4:13) Injili ya leo yaonesha kama vile iko nje ya mada iliyopita kutokana na maneno ya maingilio: “Baada ya maneno hayo yapata siku nane.” Ni maneno gani hayo aliyosema Yesu siku nane kabla hata ikumbushwe tena hapa? Halafu hizo siku nane zinatuhusu nini sisi?

Ndugu zangu siku nane kabla, Yesu alitoa maamuzi mazito juu ya msimamo aliojiwekea na kuufuata yeye mwenyewe katika maisha yake. Halafu akawaalika wanafunzi wake endapo wako radhi kufuata misimamo hiyo kwa vitendo. Alisema: “Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike Msalaba wake kila siku, anifuate.” Kabla ya kuamua kumfuata, yabidi mtu akae kwanza chini kujiuliza kidhati kama “Inalipa kweli kufuata maisha ya mtu huyu au kufuata maisha ya watu wengine maarufu waliofaulu katika ulimwengu huu.”  Injili ya leo ina lengo la kuwaandaa wanafunzi kutoa maamuzi mazito ya mustakabali wa maisha yao. Nasi sote tunaalikwa kufuatilia kidhati misimamo hii ya Yesu ilikomfikisha na kutoa maamuzi yetu ya maisha.

Kwa hiyo, baada ya hizo siku nane, Yesu “aliwatwaa Petro na Yohane na Yakobo.” Hawa walikuwa ni wanafunzi watatu tu kati ya wale kumi na wawili. Hii tena ni taarifa kwetu kwamba mtu huyu Yesu hakuwa mwenye mafanikio, hata kati ya wanafunzi wake, wanachukuliwa watatu tu wa kufuatana naye kwenda sehemu nyeti. Baada ya uteuzi huo“ Yesu akapanda nao kwenda mlimani.” Hapa tena halitajwi jina la mlima kama inavyotajwa katika Injili nyingine (wengine wanasema ulikuwa mlima Tabor), kwa hoja kwamba, katika nafasi hii mlima huu si wa kijiografia au pahala, bali ni hali ya watu wachache, walio pamoja na Yesu ndiyo wanayofaulu kuing’amua. Hao wachache ndiyo wanaoingia katika mtazamo wa mambo kwa jicho la Kimungu. Kwa hiyo binadamu wote tunazungukazunguka tu humu ulimwenguni, lakini ni binadamu wachache tu kati yetu ndiyo wanaobahatika kupanda mlimani wanakoweza kupata fikra tofauti na wengine wote. Yawezekana hawa wachache walikuwa wameandaliwa zaidi ili waweze kufahamu misimamo ya Yesu, tofauti na mtazamo wa kibinadamu.

Halafu Yesu“alipanda huko mlimani kuomba” Kumbe lengo la Yesu la kuwatwaa wanafunzi hawa watatu na kupanda nao mlimani lilikuwa ni kusali. Sala ni kipindi cha kiroho cha kutafakari, ndicho kilichomfanya Yesu ajigundue kuwa ana utume gani hapa duniani. Kumbe, “Ikawa katika kusali kwake sura ya uso wake ikageuka.” Sura ya Kristu iliyozama katika sala na kuingia katika fikra ya Mungu inaonesha ushindi. Hapo ndipo hata macho ya mitume yakafunguka na kuyaona mabadiliko ya uso wa Yesu. Tofauti na atu wengine walioiona sura ya Yesu kama iliyoshindwa na kufedheheka. Katika sala sura ya mtu aliyejitoa kwa ajili ya wengine inang’ara na inakuwa ya mtu aliyefanikiwa, inakuwa sura ya Mwana anayeakisi sura ya Mungu Baba yake. Sisi pia tunaweza kumwona Yesu kwa jicho la kibinadamu, kuwa ni mtu wa ajabu na mtenda miujiza lakini tukashindwa kumfuata. Kumbe kwa njia ya sala tunaweza kuiona sura yake imegeuka na tukaweza kutoa maamuzi ya kumfuata na kutoa maisha yetu kwa ajili ya wengine.

Wanafunzi walipokuwa katika kushangaa,“Na tazama, watu wawili walikuwa wakizungumza naye, nao ni Musa na Eliya.” Watu hawa wawili wanawakilisha Sheria na manabii katika Agano la kale ndiyo waliomwelewa Yesu ni nani na anao ujumbe gani. Nabii alisema: Kusudi Neno la Mungu liweze kuleta wokovu duniani ilibidi neno hilo liteseke hata kwa vile lilipambana na giza la ulimwengu lililotaka kuendeleza hali yake ya giza. Kumbe mwanga ulitaka kuleta mwanga mpya wa upendo. Kisha, “Petro na wale waliokuwa pamoja naye walikuwa wamelemewa na usingizi” Kwa kawaida tukiwa usingizini tunafumba macho kwa vile mwanga unasumbua macho. Kwa hiyo katika sala wanafunzi hawa watatu wamegundua huko kubadilika uso wa Yesu.

Wameyaelewa mapendekezo ya kujitoa maisha yao kama Yesu mwenyewe na wamepiga mahesabu ya gharama ya kumfuata wakaona ni maji marefu, ni kama mwanga mkali unaoumiza macho. Kwa hiyo wanaamua kufumba macho na kulala usingizi ili kukwepa majukumu. Hali ya wanafunzi hawa kulala-lala usingizi wanapoona matatizo mazito ya maisha ilitokea pia bustani ya Gestemani: “Alipoondoka katika kuomba kwake, akawajia wanafunzi wake, akawakuta wamelala usingizi kwa huzuni.” (Lk 22:45). Wanafunzi wanafunga macho ili wasishuhudie kile atakachokabiliana nacho mwalimu wao. Kumbe, sisi sote tunaalikwa tuwe macho. “Ni muda wa kuamka usingizini, mchana umekaribia.”

“Ikawa Musa na Eliya walipokuwa wakijitenga naye, Yesu alibaki peke yake,” ikimaanisha kuwa Agano la kale linatusaidia kumwelewa Kristo na likishamaliza shughuli ya kutuelewesha Kristu ni nani, tubaki kumtazama na kumtafakari Kristu peke yake “Watamtazama yeye waliyemchoma.” Hiki ndicho kitu tunachotakiwa kukifanya katika kipindi hiki cha kwaresima na tunapojiandaa kwa juma kuu. Tunaalikwa kutafakari sura ya Kristu katika sala. Tukisali na kuangalia matendo ya Yesu na kuyafuata katika mwanga wa mbinguni tutaweza hata sisi kugeuka uso na kupendeza. Petro akamwambia Yesu, “Bwana mkubwa ni vizuri sisi kuwapo hapa, na tufanye vibanda vitatu, – kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya – hali hajui asemalo.”  Kufanya vibada maana yake kubaki pahala pamoja bila kuondoka. Kumbe mwanafunzi wa Yesu yuko safarini daima. Petro alijikia amefika na akataka abaki hapo alitaka abaki hapo. Kumbe utimilifu wa maisha ni kutoa maisha kwa ajili ya wengine katika upendo.

“Alipokuwa akisema hayo, lilitokea wingu likawatia uvuli, wakaogopa walipoingia katika wingu hilo.” Wingu ni picha ya Mungu na ni mang’amuzi ya ndani ya mtu. Wanafunzi wanaingia katika ulimwengu wa fikra za Kimungu na katika hatima ya lengo la Mungu kama lile alilofikia Kristu. Yatubidi sisi sote kuyafuata mang’amuzi hayo, yaani kusikia sauti inayotoka uwinguni, sauti inayotuonesha safari au njia ya maisha yaliyo bora, yaliyokamilika. Sauti isemayo: “Huyu ni Mwanangu, mteule wangu msikieni yeye.” Tunatakiwa kuyasikiliza na kuyapokea mapendekezo ya Mwana anayetambuliwa na kupendwa na Baba wa mbinguni na tumfuate.  “Sauti hiyo ilipokwisha, Yesu alionekana yu peke yake. Nao wanafunzi wakanyamaza wasitangaze kwa mtu siku zile lolote katika hayo waliyoyaona.” Wanafunzi hawakuweza kutangaza chochote kwa vile hawakuelewa hatima ya maisha ya Yesu yangekuwaje na wanafunzi angewaacha-achaje.

Leo sisi tunatambua jinsi maisha ya Yesu yalivyoishia na jinsi tulivyotuachwa–achwa. Hapo ndipo tunapoweza kuelewa mantiki ya maneno yale ya maingilio ya fasuli ya leo na jinsi yanavyoelekezwa kwetu sisi “Yapata siku nane baada ya maneno hayo.” Kumbe kila siku ya nane, wakristu tunayo fursa ya kukutana katika jumuia na kusali. Hapo tunapata fursa ya kutafakari uso wa Kristu, na kuona jinsi unavyogeuka na kuwa tofauti na unavyodhaniwa kuwa kwa macho ya kibinadamu. Kila baada ya siku nane tunaalikwa kutafakari juu ya uso uliogeuka na kutukumbusha kwamba katika maisha yetu kutabaki upendo ule tulioujenga. Yote yatafutwa isipokuwa upendo ndiyo utakaodumu hapa duniani kwa sababu upendo unatoka kwa Mungu.

 

Na Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.