2016-02-19 09:53:00

Agenda 2030: Binadamu; Umaskini, Uhuru wa kuabudu; Ardhi, Makazi na Ajira


Agenda ya Maendeleo Endelevu kwa Mwaka 2030 haina budi kujikita katika mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kuendelea kupambana na umaskini kwa kuwa na sera pamoja na mikakati makini ya maendeleo, ili kuwasaidia wananchi wengi kuondokana na umaskini wa hali na kipato. Juhudi hizi hazina budi kusindikizwa na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwani athari za mabadiliko ya tabianchi zimekuwa tena ni chanzo kikuu cha umaskini kati ya watu! Hizi ni changamoto ambazo zinapaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa. 

Haya yamesemwa hivi karibuni na Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa wakati alipokuwa anachangia mada kwenye kikao cha 54 cha Tume ya Maendeleo Jamii ya Umoja wa Mataifa mintarafu mipango mipya ya maendeleo ya kijamii katika ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2016 anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine kwa kupambana fika na ukosefu wa haki msingi za binadamu; uhuru, utu na heshima ya binadamu pamoja na kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya amani. Jumuiya ya Kimataifa ijikite katika ujenzi wa utandawazi wa mshikamano, ili kukamilisha ajenda za Maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030.

Askofu mkuu Auza anakaza kusema, sera hizi hazina budi kuwa endelevu, usawa pamoja na kuwahusisha watu wengi, ili kamwe asiwepo mtu anayetengwa katika sera na mikakati hii. Lengo ni kuwa na maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kulinda utu wa mtu pamoja na kuziwezesha familia kutekeleza dhamana na majukumu yake. Ili kweli Malengo ya Maendeleo Endelevu yaweze kutekelezwa watu wanapaswa kuzingatia umuhimu wa kuwa na: makazi, fursa za ajira na ardhi ambamo wanaweza kutumia kwa ajili ya kuzalisha na kutoa huduma. Uhuru wa kidini unapaswa pia kupewa kipaumbele cha pekee, sanjari na elimu makini inayoambata haki msingi za kiraia.

Ni matumaini ya Askofu mkuu Auza kwamba, Serikali na viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wataweza kujitosa kimasomaso katika utekelezaji wa sera na mikakati ya maendeleo ili kuunga mkono juhudi za Jumuiya ya Kimataifa na utekelezaji wa sera makini za maendeleo endelevu kwa ajili ya binadamu, mafao ya wengi na jamii katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.