2016-02-18 12:05:00

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya II ya Kwaresima Mwaka C


Uso ni ukaribisho wa hali ya ndani ya mtu. Daima mtu anapotokea mbele ya wengine watu umtathimini kwa haraka kupitia mwonekano wa uso wake. Mtunga Zaburi katika dominika ya leo anaonesha hamu ya kuuona uso wa Mungu kwa sababu ni mng’ao na utukufu. Zaburi hiyo ambayo inaendelea kukaririwa katika wimbo wa katikati inaonesha matumaini ya yule anayekimbilia uso wa Mungu. Yeye anakuwa daima hana woga wala hofu. Pale anapokuwa katika hatari hubaki akimlilia Mungu na kusema: “umekuwa msaada wangu, usinitupe, wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu”. Mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu unatualika kutoka katika giza la uvuli wa mauti na kuuendea mng’ao wa utukufu wa Mungu. Uwepo wa Mungu mahali popote unaonekana katika utukufu wake. Huu ndiyo mwaliko tunaoupata tunapoadhimisha Dominika ya 2 ya Kwaresima.

Katika somo la Kwanza tunaona Mungu anajitokeza katika alama ya moto na kufanya agano na Baba yetu wa imani Ibrahimu. Huo ulikuwa ni uhakikisho wa uwepo wake na ulinzi wake na pia uthibitisho kwa Agano lake alilofunga naye. Somo la Injili ni ukamilifu wa uwepo huo wa Mungu katika utukufu wake. Kristo ambaye ni utimilifu wa ufunuo wa Mungu kwetu anajidhihirisha mbele ya wafuasi wake. Anawaonjesha ile hali ya utukufu ambayo imo ndani mwake na ambayo anataka nasi tuipokee na kuitwa wana wapendwa wa Mungu. Sauti ya Baba inamtambulisha Kristo ikisema: “huyu ni mwanangu mteule wangu, msikieni yeye”. Ni sauti inayothibitisha ufunuo wa huruma hii ya Mungu kwetu kwa njia ya Yesu Kristo na kutualika kwamba ni kwa njia ya kumsikiliza Yeye tu ndipo tutakapopata hadhi ya kuitwa watoto wa Mungu.

Mungu anatuangazia akili zetu katika hali yoyote ya maisha kusudi kuyapokea yote kwa hekima yake kuu. Huo ndio utukufu wa Mungu anatupatia tunapomkimbilia na kuufanya uwepo wake uwe kati yetu daima. Msalaba wa Kristo unaeleweka tu katika namna hii na utukufu wake unatung’aria kwa njia hii. Akili za kiulimwengu zinatupeleka kupingana na mapenzi ya Mungu na hivyo tunapolalia huko tunauona ni mzigo na uchungu. Hii ni kwa sababu tu mwanadamu anapotaka uhuru wa kujitenga na Mungu anaingia katika maangamizi na uwepo wa Mungu huwa ni tishio kwa uhuru wake aliojitengenezea.

Kristo ameng’aa sura sababu maisha yake yalikuwa yamejaa uwepo wa Mungu, yaani aliyapokea yote na kuyaelewa katika hekima ya kimungu na si hekima ya kibinadamu. Maisha yake yote ya hadarani yanalishuhudia jambo hili. Naye pia alisema: “chakula changu ndicho hiki: niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake” (Yoh. 4:34). Hilo ndilo tu lililomtia nguvu na kumpa maana ya uwepo wake kati yetu. Baba yetu katika imani Ibrahimu aliuona utukufu wa Mungu katika moto kwa sababu tu alikuwa na imani kuu juu ya ulinzi na wema wa Mungu ambao aliuonja katika namna ya ajabu kama jibu kwa imani yake kuu kwa Mwenyezi Mungu.

Utimilifu wa ufunuo wa Mungu katika Kristo unafikiwa kwa Fumbo la Pasaka. Kwa mateso, kifo na ufufuko wake, Bwana wetu Yesu Kristo anafikia kilele cha huruma na mapendo ya Mungu na anaudhihirisha utukufu wake. Utukufu huo unaonekana pale tu anapokuwa tayari kuitimiliza “ndiyo” yake kwa Mungu, yaani pale anaposema “Baba! mapenzi yako yatimizwe”. Hili ndilo somo kubwa tunalojifunza katika msalaba wa Kristo, yaani, kuyatii mapenzi ya Mungu katika hali zote hata kuwa tayari kuutoa uhai wako. Utii huu hauishii tu hewani, bali utupeleka katika utukufu. Kwa Kristo hili limedhihirishwa na Mtume Paulo anapowaandikia Wakristo wa Fililipi anawaambia: “kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, na vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi”.

Dhambi inatufanya kuwa mbali na Mungu. Mtume Paulo anaonya tena kwa ukali kidogo katika somo la pili kwamba wale ambao hawaikimbilii nuru hii ya Mungu “ni adui wa msalaba wa Kristo; mwisho wao ni uharibifu, mungu wao ni tumbo, utukufu wao u katika fedhea yao, waniayo mambo ya duniani”. Anaendelea mtume Paulo kufafanulia lile tutakalopokea kwa kuuendea utukufu wa Mungu kwa njia ya Yesu Kristo. Yeye Kristo ndiye “atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu”. Katika kipindi hiki cha Kwaresima tunapoalikwa kufanya toba na kumrudia Mungu basi tutiwe nguvu na karama hiyo ya kimbingu tutakayoipokea.

Mwanadamu anapotenda kadiri ya mapenzi ya Mungu anakuwa anatenda au anauweka ulimwengu katika namna yake tangu uumbwaji na jinsi Mwenyezi Mungu alivyokusudia uwe. Yeye aliuumba ulimwengu vizuri na akamkabidhi mwanadamu autunze na kuuratibu. Utukufu wa Mungu unaonekana pale tu yote yanavyokuwa katika uhalisia wake, yaani, pale kila kitu kinavyokwenda kadiri kilivyopangwa na mwenyezi Mungu kwa hekima yake ya ajabu. Lakini pale adui shetani alipomtoa mwanadamu katika uso wa Mungu ndipo huyu mwanadamu alipoanza kujifanyia mambo yake bila Mungu na daima yamekuwa yanamuingiza katika giza na mahangaiko. Uwepo wa utukufu wa Mungu unatoweka katika maisha yake.

Tunapotafakari juu ya nafasi hiyo tunayotayarishiwa ni vema basi kutambua pia hitajiko muhimu la kuifikia hali hiyo. Mwinjili Luka anatuambia kwamba: “ikawa katika kusali kwake sura ya uso wake ikageuka, mavazi yake yakawa meupe, yakimetameta”. Hapa tunaona nafasi ya sala katika kuyapokea mapenzi ya Mungu. Kristo anakuwa ni mfano kwetu. Dominika iliyopita alilidhihirisha hili. Kristo alikuwa katika sala na mafungo kwa siku arobaini na anapokutana na majaribu ya shetani alikuwa jasiri kusema: “mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo kinywani mwa Mungu. Yapo maeneo mengi ambapo tunaona Kristo anavishinda vishawishi vya shetani na kutanguliza daima mapenzi ya Mungu.

Sala humuunganisha Mungu na mwanadamu. Katekisimu ya Kanisa Katoliki namba 2259 inatuambia kwamba: “Sala ni kuinua akili na mioyo yetu kwa Mungu au ni maombi ya mambo mema toka kwa Mungu” na inaendelea kukazia kwamba “unyenyekevu ni msingi wa sala”. Hapa tunaona kwamba tendo la sala linatuinua na kutuunganisha na Mungu na katika hali hiyo ya kuunganika na Mungu tunaitambua nafasi yetu mbele yake kama viumbe, tunajinyenyekeza na kumtegemea yeye kutupatia mema yote. Ni nini zaidi tutakachopata kutoka kwa Mungu, kilicho chema zaidi ya uwepo wake katika utukufu wake? Tukumbuke kwamba “kabla ya utukufu hutangulia unyenyekevu” (Mith 15:33).

Kipindi hiki cha Kwaresima ni mwaliko wa kuutafuta uso wa Mungu. Na ndiyo maana mzaburi katika antifona ametualika kwa kutuambia: “Moyo wangu umekuambia, Bwana, uso wako nitautafuta. Usinifiche uso wako”. Ninawalika leo hii, tunapofanya bidii ya ya toba ili kumrudia Mungu na kuuona utukufu wake tumtafute katika kuyatimiza mapenzi yake. Na tutambue kuwa sisi peke yetu bila uwepo wake mara nyingi tunaanguka. Hivyo daima tumwalike ili awe nasi kwa njia ya sala zetu. Na hivyo tukumbuke pia tendo la kusali ambalo tunakumbushwa sana katika kipindi hiki cha Kwaresima. Huruma yake Mwenyezi Mungu imekwisha tung’aria. Ni wajibu wetu sasa kujongea katika utukufu huo wa Mungu.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.