2016-02-18 15:33:00

Ombeni zawadi ya chozi na toba ili kuona na kuguswa na mahangaiko ya watu!


Utukufu wa Mungu ni maisha ya watoto wake anayewaona wakikua na kusonga mbele kama ilivyokuwa kwa Mji wa Ninawi baada ya kupata mafanikio makubwa, ukaanza kuharibika kutokana na unyonyaji, uhalifu na ukosefu wa haki. Nabii Yona akatumwa na Mwenyezi Mungu ili kuwatangazia wananchi wa Ninawi hasira ya Mungu, ili waweze kuwa tayari kutubu na kumwongokea Mungu ili kuondokana na utamaduni wa kifo, mateso na dhuluma; mambo yaliyowafunga macho na kushindwa kuona ubaya na dhambi iliyokuwa inawaandama. Nabii Yona akawafungua macho na kuwazindua kutoka usingizini, tayari kuona na kuambata huruma ya Mungu katika maisha yao.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 17 Februari 2016 wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Ciudad Juàrez, Mexico kwa kusema kwamba, huruma ya Mungu inafukuzia mbali hali dhambi kwa kumwajibisha binadamu, ili kuweza kujikita katika wema kwani huruma ya Mungu inalenga kumfunda mtu kutoka katika undani wa maisha yake, kielelezo cha Fumbo la huruma ya Mungu. Huu ni mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu; kwa kuona madhara ya dhambi, tayari kufanya marekebisho. Huruma inaingia katika ubaya, ili kuleta mabadiliko ya kweli kama ilivyotokea kwa wananchi wa Ninawi, waliotubu na kuwa na matumaini mapya. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni muda muafaka wa kutenda, ili kubadilika;  kurekebisha ili kuwa na mwelekeo mpya zaidi unaojikita katika wongofu wa ndani, ili kurekebisha yale yanayowadhulu kama jamii ya watu au kuwadhalilisha kama binadamu.

Huruma ya Mungu inawasaidia waamini kuona ya sasa na kuwa na matumaini ya kile ambacho ni safi na chema, lakini kimejificha kwenye sakafu ya moyo wa binadamu kwani huruma ya Mungu ni ngao na nguvu ya watu wake. Nabii Yona aliwasaidia watu kuona dhambi zao, wakatubu na kulilia haki ya Mungu kwa kusikitika kutoka na madhulumu yaliyokuwa yanatendeka. Mchozi yakawasaidia kujikita katika wongofu wa ndani; yakawasafisha na kuwafumbua macho kuona mzunguko wa dhambi na mahangaiko ya jirani zao. Ni machozi yaliyowaletea wongofu wa ndani, changamoto kwa waamini kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu hasa wakati huu wa Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Waamini waombe zawadi ya chozi na toba ili kuona mateso na mahangaiko ya watu. Eneo hili kuna wakimbizi wanaokumbana na ukosefu wa haki msingi za binadamu; wanaogezuwa na kupelekwa utumwani; wanaotekwa nyara na kutumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, uhamiaji ni changamoto ya kimataifa inayoshuhudia idadi kubwa ya watu wenye nyuso na majina yao; wenye historia na familia zao. Ni watu wanaosukumwa na umaskini, vita, biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na uhalifu wa magenge. Waathirika wakuu ni maskini na vijana, wasichana na wanawake. Waamini wawe na ujasiri wa kuomba zawadi ya toba na wongofu wa ndani; zawadi ya machozi na mioyo wazi, kama ilivyokuwa kwa wananchi wa Ninawi ili kuwa na huruma kwa wale wanaoteseka, ili kusiwepo tena vifo vya watu wasiokuwa na hatia.

Huruma ya Mungu iwaletee watu toba na wongofu wa ndani, tayari kukumbatia wokovu sanjari na kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki za wakimbizi na wahamiaji sanjari na zawadi ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo. Wadau mbali mbali wanaotekeleza dhamana hii kwa ari na moyo mkuu ni Manabii wa huruma ya Mungu na vyombo vya Kanisa linalofungua mikono yake ili kuwapokea na kuwahudumia watu hawa. Hiki ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani; muda muafaka wa huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kuwasalimia waamini waliokuwa wanafuatilia Ibada hii ya Misa wakiwa upande wa pili wa mpaka kati ya Marekani na Mexico, kwenye Uwanja wa Chuo kikuu cha El Paso, maarufu kama Sun Bowl, waliokuwa wakiongozwa na Askofu Mark Seitz. Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano, yamewezesha waamini kutoka pande hizi mbili kusali, kuimba na kuadhimisha kwa pamoja upendo wa huruma ya Mungu unaovuka mipaka ya nchi, ili wote waweze kujisikia kuwa ni familia na jumuiya moja ya Kikristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, 

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.