2016-02-18 12:18:00

Mtu aliyeteseka na kuonja kuzimu, anaweza kuwa ni Nabii wa Jamii yake!


Hija ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Gereza kuu la Ciudad Juàrez, Mexico, Jumatano tarehe 17 Februari 2016 imekuwa na mvuto wa pekee, alipokutana ili kuzungumza na kusali na wafungwa wa gereza hilo, tukio ambalo limerushwa moja kwa moja na Tume ya haki za binadamu nchini Mexico kwenye magereza 389 ya Mexico, yanayohifadhi wafungwa zaidi ya 254, 000. Baba Mtakatifu alipofika gerezani hapo moja kwa moja alikwenda kusali kwenye Kikanisa cha gereza na kuwashukuru askari magereza kwa kazi kubwa wanayoifanya hata kama wakati mwingine haionekani na wengi.

Baba Mtakatifu amelizawadia gereza hili Msalaba wa kioo, kuonesha hali tete ambayo Kristo Yesu amemwonesha mwanadamu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu. Kwa njia ya Fumbo la Msalaba, akawakomboa wanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na kuwafungulia lango la huruma na matumaini mapya. Amewaalika kufanya tafakari ya kina kuhusu Fumbo la Msalaba, ili waweze kuonja ndani mwao matumaini na ufufuko katika maisha yao.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa wafungwa hawa amewashukuru wote waliomwezesha  kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu pamoja na wafungwa gerezani hapo. Maneno yao yanagusa matumaini, uchungu wa moyo, wasi wasi hata pengine na maswali mengi yasiyokuwa na majibu. Lango la kwanza la Huruma ya Mungu lilifunguliwa na Mwenyezi Mungu kwa kumtuma Mwanaye wa Pekee, Kristo Yesu. Baba Mtakatifu akarudia tendo hili kwa kufungua lango la maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu ni fursa ya kuwaimarisha waamini kuwa na imani, tayari kuambata huruma ya Mungu inayofunuliwa na Kristo Yesu kwa wote. Maadhimisho haya miongoni mwa wafungwa ni mwaliko wa kufanya hija ya pamoja ili kuvunjilia mbali mnyororo wa uhalifu na uvunjaji wa sheria. Kwa miaka mingi watu walidhani kwamba, kwa kuwafunga na kuwatenga wahalifu na wavunja sheria, wangeweza kutatua matatizo ya kijamii na kusahau kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na maisha ya watu bila kusahau familia zao, ambazo pia zimeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na mnyororo wa uvunjaji wa sheria.

Baba Mtakatifu anasema, huruma ya Mungu inawaambata wote hata wale ambao wako magerezani, katika hali ya ukimya na kutowajibika, mambo ambayo wakati mwingine yanachangia kwa kiasi kikubwa, utandawazi wa kutojali wala kuguswa na mahangiko ya wengine; ni mwelekeo wa utamaduni usiojali zawadi ya maisha na kielelezo cha jamii ambayo taratibu imewasahau watoto wake. Toba na wongofu wa ndani anakaza kusema Baba Mtakatifu unapaswa kuanzia kwenye barabara na mitaa, ili kuganga na kuponya madonda ya kijamii, kwa kurekebisha mahusiano na mafungamano ya kijamii katika medani mbali mbali za maisha. Kwa kudumisha utamaduni unaolenga kuwakinga wananchi na majanga wanayoweza kukumbana nayo katika maisha yao. Inasikitisha kuona kwamba, hata baada ya watu kufungwa magerezani lakini bado watu wanaendelea kufanya uhalifu. Usalama wa raia na mali zao hauwezi kudumishwa kwa kuwafunga watu magerezani, bali kwa kufanya upembuzi yakinifu kwa kuangalia miundo mbinu na mambo ambayo yanachangia ukosefu wa usalama wa raia na mali zao.

Baba Mtakatifu anasema, matendo ya huruma kama yalivyohubiriwa na Kristo Yesu ni kielelezo cha huruma ya Mungu kwa waja wake na hivyo inakuwa ni kanuni maadili kwa jamii inayotaka kujikita katika mahusiano na mafungamano mema ya kijamii, kwa kuwahusisha watu wote bila kuwatenga wala kuwanyanyasa, ili kuwapatia nafasi ya kuganga na kuponya madonda yao ya ndani. Uponyaji wa kweli unajikita katika elimu makini kwa watoto; kwa kuwa na fursa za ajira zinazowasaidia watu kutekeleza majukumu yao ya kifamilia; kwa kuwa na nafasi za mapumziko na starehe, bila kusahau kuwashirikisha watu katika masuala ya kijamii; kwa kuwapatia huduma bora za afya na mahitaji yao msingi. Huu ndio mwanzo wa mchakato wa ujenzi wa mafungamano bora ya kijamii.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu miongoni mwa wafungwa iwe ni nafasi kuondokana na mambo ya kale, kwa kujifunza kufungua malango ya maisha kwa siku za usoni kwa kutambua kwamba, inawezekana kufanya yote mapya. Ni mwaliko wa kuinua kichwa juu, kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuwa na uhuru kamili, kwa kutambua mapungufu yao yaliyopelekea hata wakajikuta wakiwa gerezani. Jubilei ni chachu ya matumaini kwa maisha mapya baada ya mateso na mahangaiko ya ndani, tayari kuondokana na upweke hasi katika maisha.

Kwa kutekeleza adhabu yao magerezani, wafungwa wameguswa na nguvu ya machungu na dhambi; lakini mbele yao wanayo pia nguvu ya ufufuko na maisha mapya; nguvu ya huruma ya Mungu inayowasindikiza katika mwelekeo mpya. Iwe ni fursa ya kuendeleza mazungumzo na majadiliano na ndugu, jamaa na marafiki, kwa kuwasimulia mang’amuzi yao, ili kudhibiti mnyororo wa vitendo vya uhalifu na upweke hasi. Kwa mtu aliyeteseka sana, huyo ameonja maisha ya kuzimu na kutokana na machungu haya, anaweza kuwa kweli ni Nabii ndani ya jamii. Wafungwa wanapaswa kuendelea kupyaisha maisha yao, ili amani na utulivu viweze kupatikana tena, kwa kutambua kwamba, binadamu wote ni wadhambi na wanahitaji huruma na upendo wa Mungu.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, hata yeye katika maisha yake ameguswa na mapungufu ya kibinadamu, lakini Kristo Yesu, akamsamehe na kumpatia tena fursa ya kuanza upya na kwamba, ni kwa njia ya neema yake, anaweza kusonga mbele pasi na kutumbukia tena katika dhambi za mazoea. Daima machoni pake anaiona huruma ya Mungu katika maisha yake; huruma inayomwezesha kusonga mbele kwa matumaini zaidi. Anawashukuru wote wanaojisadaka kwa ajili ya huduma kwa wafungwa magerezani, ili kuwatangazia Injili ya huruma ya Mungu na kwamba, watu wanategemeana na kukamilishana katika hija ya maisha. Mwishoni, wote wamesali katika ukimya, ili kuomba huruma ya Mungu katika maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.