2016-02-18 15:45:00

Mexico imeonja huruma na upendo wa Mungu!


Askofu Torres Campos wa Jimbo Katoliki Ciudad Juarez, Mexico, wakati wa Ibada ya Misa takatifu niliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye mpaka wa Mexico na Marekani, Jumatano, tarehe 17 Februari 2016, amemshukuru Baba Mtakatifu kwa kuandika historia mpya katika maisha ya wananchi wa mji huo, ambao wameguswa na kutikiswa na magumu ya maisha; ambayo kwa hakika yameacha madonda makubwa katika familia. Hawa ni watu ambao wameshuhudia na kutikiswa na vita na uchu wa mali na madaraka.

Uwepo wa Baba Mtakatifu kati yao ni alama ya matumaini na baraka kutoka kwa Mungu kama ilivyokuwa kwa Yesu Msamaria mwema aliyejinyenyekesha ili kufunga na kuganga madonda ya maisha ya mwanadamu! Ujumbe wa Baba Mtakatifu uumevuka mipaka ya Mexico na kuwafikia hata wale waliokuwa nchini Marekani. Na kwa njia ya Ibada hii ya Misa Takatifu, Papa Francisko alikuwa anahitimisha rasmi hija yake ya kitume nchini Mexico kama mmissionari wa huruma ya Mungu na mjumbe wa amani.

Baba Mtakatifu amebahatika kukutana na kuzungumza na watu wema, wenye nguvu na wa wazi wanaotaka kusonga mbele kwa imani na matumaini katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Amewapatia ujasiri wa kumwilisha huruma na upendo wa Mungu kwa jirani bila kumtenga mtu awaye yote!. Uwepo na ushuhuda wa Baba Mtakatifu Francisko kati yao anasema Askofu Torres Campos kuwa utaendelea kuchafua kutoka katika sakafu ya maisha na mioyo yao. Amekuwa kweli ni shuhuda wa Injili ya furaha na matumaini kwa wananchi wa Mexico na dunia nzima.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.