2016-02-18 14:50:00

Gereza ni mahali ambapo kuna kilio kikuu cha huruma na haki!


Askofu msaidizi Andrès Vargas Penà, Mwenyekiti wa Tume ya Magereza ya Baraza la Maaskofu Katoliki Mexico, katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kuzungumza na wafungwa wa Gereza kuu la Ciudad Juàrez, Mexico, Jumatano tarehe 17 Februari 2016, amempongeza Baba Mtakatifu kwa kuwapelekea wafungwa furaha ya Injili; maeneo ambayo yana kilio kikuu cha huruma na haki. Mexico kuna idadi kubwa ya wafungwa ambao wako magerezani matokeo ya biashara haramu ya binadamu, dawa za kulevya; biashara haramu ya silaha, rushwa na ufisadi. Mambo yote haya yana madhara makubwa katika maisha ya kijamii na waathirika wakuu ni watu wasiokuwa na hatia, watoto, vijana, maskini na familia husika.

Askofu Andrès anasema yote haya ni matokeo ya ukosefu wa haki na usawa wa kijamii; lakini bado kuna Wainjilishaji wanaoendelea kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa njia ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu; mahubiri na shuhuda za huduma makini kwa familia na wale wote ambao hawana tena uhuru. Ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa wafungwa ni chachu ya mageuzi, ili kuhakikisha kwamba, huruma, haki na msamaha vinatendeka sanjari na kutoa adhabu mbadala ili magereza yasiwe ni mahali pekee pa kuwafunza watu. Wananchi wa Mexico wanaendelea kumwombea Baba Mtakatifu ili huruma ya Mungu anayoendelea kuitangaza na kuishuhudia, iwe ni kwa ajili ya ustawi na mafao ya watu na Kanisa katika ujumla wake.

Wafungwa wamemwambia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, uwepo wake miongoni mwao ni chachu  ya kukimbilia huruma ya Mungu na matumaini kwa kutambua kwamba, wao pia ni binadamu na kwamba, ndani mwao bado wanajisikia ile ari na mwamko wa kukombolewa, kwani magerezani wanapata changamoto za maisha ya kiroho na kimwili; wanakumbana na upweke hasi. Wanapohukumiwa, wanashikwa na huzuni kwa kujiuliza maswali mengi yasiokuwa na majibu. Wafungwa hawa wamemhakikishia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, uwepo wake miongoni mwao, umeacha chapa ya kudumu katika sakafu za mioyo yao. Kwa mara nyingine tena, wameonja furaha na matumaini mapya; mambo yanayorutubisha imani na matumaini ya kurejea tena kwenye familia! Wafungwa wanasema, uwepo wa Baba Mtakatifu umewasaidia kuonja huruma ya Mungu katika maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.