2016-02-18 15:56:00

Familia ya Mungu Mexico, asanteni sana!


Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake wakati wa kufunga vilago vya hija yake ya kitume huko Ciudad Juàrez, amewashukuru wadau mbali mbali waliofanikisha hija yake ya kitume nchini Mexico. Kuna maelfu ya watu waliofanya kazi kubwa katika hali ya ukimya pasi na makuu; wakajisadaka na kujitosa kimasomaso bila ya kujibakiza, ili kufanikisha maadhimisho haya ya kifamilia. Baba Mtakatifu anawashukuru wote hawa kwa kusema kwamba, amejisikia kweli yuko nyumbani, kiasi cha kuadhimisha siku kuu inayojikita katika matumaini kwa familia kubwa ya Mexico.

Baba Mtakatifu anawashukuru kwa kumfungulia malango ya familia na taifa lao, ili kuonja udugu na upendo na uwepo wa ajabu wa Mwenyezi Mungu katika maisha ya watu, hasa zaidi miongoni mwa maskini. Kuna kundi kubwa la wamissionari na mashuhuda wa huruma ya Mungu wanaoendelea kujisadaka ili kuwapatia watu matumaini na mwanga mpya wa maisha; wao ni mashuhuda wa kesho na ndoto ya maisha mapya. Baba Mtakatifu amewaombea wananchi wa Mexico ili Bikira Maria aendelee kuwatembelea na kuwasaidia, ili kweli waweze kuwa ni wamissionari na mashuhuda wa huruma na upatanisho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.