2016-02-17 11:48:00

Vijana ni jeuri na utajiri wa Mexico!


Baba Mtakatifu Francisko amekutana na umati wa vijana waliokuwa wakisali, wakiimba na kucheza, kwenye Uwanja wa michezo wa Morelia, Mexico, Jumanne, tarehe 16 Februari 2016, huu ni ushuhuda wa nguvu na jeuri ya vijana; shangwe na furaha ya wananchi wa Mexico na kwamba hawa ni hazina na rasilimali kubwa kwa ustawi na maendeleo ya Mexico. Baba Mtakatifu amewakumbusha vijana kwamba, wao ni utajiri na matumaini ya Mexico; changamoto kubwa iliyoko mbele ya Mexico ni kuhakikisha kwamba, vijana wanaheshimiwa na kuthaminiwa pamoja na kuwajengea matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi, kwa kuanzia nyumbani na katika ngazi ya mtu binafsi.

Baba Mtakatifu anasema, kitisho kikuu cha matumaini ni pale mtu anapojisikia kwamba, hakuna mtu anayemthamini wala kujali uwepo wake, kiasi cha kujisikia kuwa kama “soli ya kiatu”, mambo yanayoacha machungu makubwa katika maisha na mioyo ya vijana wengi. Baba Mtakatifu anawaonya vijana kutodhani kwamba, wanakuwa na thamani kubwa mbele ya watu kwa kuvaa mavazi ya gharama; kwa kuwa na fedha na mali nyingi; lakini katika undani wa mtu anajikuta ni maskini, huku akitindikiwa upendo wa dhati. Kuna baadhi ya vijana wanadhani kwamba, wakiwa na fedha wanaweza kununua kila kitu wanachotamani katika maisha; wanaweza kununua hata upendo kutoka kwa wengine. Vijana wanadhani wakiwa ni magari ya fahari, hapo kila mtu atawavulia kofia na kuwaabudu; mambo ambayo ni hatari sana kwa utambulisho, utu na maisha ya vijana!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, vijana wa Mexico ni jeuri na utajiri wa Kanisa. Wakati mwingine, inakuwa ni vigumu kwa vijana kuonja dhana hii ikiwa kama kila wakati wanapoteza vijana wenzao, ndugu na jirani kutokana na biashara na matumzi haramu ya dawa za kulevya; makundi ya kihalifu yanayoendelea kupandikiza hofu na mashaka ya maisha. Ni vigumu kuonja utajiri huu, ikiwa kama vijana wengi hawana fursa za ajira, nafasi ya masomo na majiundo makini; pale haki zao zinapotelekezwa na matokeo yake wanajikuta wakiwa wamepigwa bumbuwazi. Ni vigumu kwa vijana kujisikia kuwa kweli ni utajiri wa taifa, ikiwa kama vijana hawa wanatumiwa kwa ajili ya kutosheleza tamaa za watu.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema, pamoja na matatizo na changamoto zote hizi, kamwe hachoki kusema, vijana ni utajiri wa Mexico; anayasema haya kwani ana imani kwa Kristo Yesu anayeendelea kupyaisha maisha na matumaini ndani mwake; anayewaangalia kwa jicho la huruma na mapendo; anayeendelea kuwaalika ili kutubu na kumwongokea katika maisha; pale wanapokutana naye anawapatia fursa ya kuwa watu wema zaidi kwa kukataa kishawishi cha kuwa “mateja” ya biashara na dawa haramu za kulevya na wale wote wanaokumbatia utamaduni wa kifo! Kwa kumwambata Kristo, Baba Mtakatifu anawaambia vijana licha ya umaskini, kutengwa na ukosefu wa fursa mbali mbali, bado wanaweza kuwa na matumaini ya kupata elimu na majiundo makini. Yesu Kristo anawajalia jeuri, ari na nguvu ya kujisikia kuwa kweli vijana ni muhimu katika maisha ya jamii.

Neno la matumaini ambalo Baba Mtakatifu Francisko amewaachia vijana wa Mexico ni Yesu Kristo, mwaliko wa kukumbatia Msalaba wake, pale wanapohisi kwamba, dunia yote imewaangukia. Kwa kuambatana na Yesu daima, watangundua kwamba, kweli wao ni chumvi na mwanga wa maeneo yao wanamoishi. Yesu anawapenda jinsi walivyo hata kama hawana magari ya fahari na fedha, lakini watambue kwamba, Yesu anawapenda na kuwathamini; anawakumbatia na kuwasindikiza katika hija ya maisha yao ya kila siku, ili waweze kujisikia kuwa ni sehemu ya familia na jamii inayowazunguka.

Yesu anaendelea kuwaita vijana wengi kama alivyofanya kwa Mtakatifu Juan Diego, ili kujenga madhabahu ya jumuiya na familia; kwa kujisikia kuwa kweli ni raia wanaojenga familia kubwa ya Mungu; tayari kutoka kifua mbele ili kuwatangazia na kuwashuhudia vijana wengine kwamba, wao ni utajiri mkubwa wa Mexico, ambao kamwe hawezi kutoswa hivi hivi tu! Yesu anawaita kuwa ni wafuasi wake, ili kupata utimilifu wa maisha. Baba Mtakatifu anawambia vijana wanapokuwa katika mashaka, wathubutu kumwangalia Kristo Yesu, watatambua thamani ya ujana wao kuwa ni utajiri mkubwa kwa Mexico.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.