2016-02-17 13:56:00

Vijana nchini Mexico wanataka kujenga familia, amani na matumaini


Kardinali Alberto Suàrez Inda, Askofu mkuu wa Morelia, Mexico amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na vijana wa Mexico, Jumanne tarehe 16 Februari 2016 kwenye Uwanja wa Morelia kwa kusema kwamba, Mexico ni nchi ya watu wenye furaha na matumaini; kuna mipasuko ya kijamii kwa vile kila mtu anajisikia kuwa ni nahodha; lakini wananchi wanataka kuona umoja na mshikamano; furaha na utulivu kama ilivyokuwa kwa kijana Juan Diego alipotokewa na Bikira Maria wa Guadalupe.

Familia ya Mungu nchini Mexico inaendelea kusali ili kumwombea Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake; kwa kuendelea kuwaonesha faraja na  huruma ya Mungu inayofumbatwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Wanamshukuru kwa mbegu njema anayopandikiza kati yao ambayo itakutana na udongo mzuri na kwa neema ya Mungu itaweza kuzaa matunda mengi nyoyoni mwao.

Kwa upande wake, Askofu  Hèctor Luis Morales Sanchez, mwenyekiti wa idara ya utume wa vijana, amemhakikishia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, wanataka kuendelea kujipyaisha katika maisha na utume wao, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu; kwa kutambua kwamba, hata wao wamekombolewa kutoka katika dhambi, huzuni na utupu wa maisha ya ndani sanjari na upweke hasi. Kanisa linatambua utakatifu wa vijana wanaopaswa kuheshimiwa na kuonjeshwa huruma na upendo wa Mungu sanjari na kushirikiana nao.

Baraza la Maaskofu Katoliki Mexico ili kukuza utume kwa vijana wameanzisha Siku ya Vijana Kitaifa, Msalaba wa Kimissionari uliobarikiwa na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na vijana pamoja na kuwa na mkakati makini wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya kuwainjilisha vijana: kiroho na kimwili. Maaskofu wanamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa ushuhuda wa maisha na utume wake na kwamba, wanaendelea kumwombea ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Gudalupe.

Vijana katika shuhuda zao, wamemwambia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, wanahitaji familia, amani; wanapenda kuonesha vipaumbele katika maisha yao na kumwomba neno la matumaini katika maisha yao. Vijana wanatambua kwamba, familia ni shule ya upendo, mshikamano na maisha; ni mahali ambapo watu wanajifunza tunu msingi za maisha ya kiroho na kimwili zinazomuunda mtu mzima. Familia ni kitovu cha usalama na uhakika wa maisha. Kwa bahati mbaya, vijana wa Mexico wanakosa dhana na mwelekeo huu wa familia kwani wanapata mifano mibaya ya kifamilia na kwenye vyombo vya habari; lakini wao wanataka kujenga familia inayoambata huruma ya Mungu!

Vijana wanataka kuona amani ikatawala akili na mioyo yao; kuona maendeleo pamoja na kuzitegemeza familia zao; kuona mchakato wa Injili ya uhai, haki, amani na upatanisho vikimwilishwa katika maisha ya watu; ili kujenga na kudumisha utamaduni wa usawa na kuheshimiana; tayari kutoka kifua mbele kwa ajili ya kushiriki katika Uinjilishaji mpya, ili kuadhimisha imani inaoshuhudiwa katika uhalisia wa maisha ya mtu aliyekutana na Kristo Yesu, ili kuonja msamaha, umoja na udugu. Vijana wanakabiliwa na ukosefu wa fursa za ajira, elimu na majiundo makini; matokeo yake wamegeuka kuwa ni “mateja” wa biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; Uhalifu na utumwa mamboleo bila kusahau utekaji nyara wa watu. Vijana wanataka amani.

Vijana wanasema, wanapenda kuendeleza mema na mazuri yanayojikita katika Jamii ya Mexico; kwa kuendelea kusoma zaidi, ili kuchangia katika ustawi na maendeleo ya nchi; kujenga na kudumisha utamaduni wa mawasiliano kwa kusikiliza na kuwathamini wengine badala ya kumezwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ambayo wakati mwingine inawaacha wakielea kwenye ombwe la upweke! Vijana wanataka kushinda woga na hofu, tayari kutoka kifua mbele kushiriki katika mchakato wa maendeleo ya jamii. Vijana wanatambua kwamba wao ni matumaini ya Mexico, chachu ya Uinjilishaji mpya na kwamba, wakishikamana na Kristo Yesu kwa hakika watapata utimilifu wa maisha kwani Yesu ni njia, ukweli na uzima na chemchemi ya matumaini mapya!

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.