2016-02-17 15:26:00

Padre Richard Kuuia Baawobr ateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Wa, Ghana


Baba Mtakatifu Francisko amekubali ombi lililowasilishwa kwake na Askofu Paul Bemile wa Jimbo Katoliki Wa, Ghana la kung’atuka kutoka madarakani kadiri ya Sheria za Kanisa namba 401 § Ibara ya 1. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Richard Kuuia Baawobr, Mmissionari wa Afrika kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Wa, Ghana. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule alikuwa ni Mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Afrika.

Askofu mteule Richard Kuuia Baawobr, alizaliwa tarehe 21 Juni 1959, Jimboni Wa, Ghana. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa na kikasisi, tarehe 18 Julai 1987 akapewa Daraja Takatifu. Tangu wakati huo, amekuwa ni Paroko msaidizi kwenye Parokia la Livulu, Jimbo kuu la Kinshasa, DRC. Kuanzia mwaka 1991 hadi mwaka 1996 alikuwa masomoni kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian akichukua masomo ya Sayansi ya Biblia na baadaye akatunukiwa Shahada ya Uzamivu katika somo la Taalimungu Biblia.

Kunako mwaka 1996 hadi mwaka 1999 akatumwa nchini Tanzania kama mlezi kwenye nyumba ya Shirika la Wamissionari wa Afrika, huko Kahangala, Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania. Kuanzia mwaka 1999 hadi mwaka 2004 akawa ni Mkurugenzi wa nyumba ya malezi huko Tolosa, nchini Ufaransa. Kunako mwaka 2004 hadi mwaka 2010 akachaguliwa kuwa ni kati ya washauri wakuu wa Shirika la Wamissionari wa Afrika, maarufu kama “White Fathers”.

Kunako mwaka 2010 akachaguliwa kuwa Mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Afrika, mwafrika wa kwanza kuchaguliwa kuliongoza Shirika hili tangu kuanzishwa kwake! Amekuwa pia ni Makamu mkuu wa Taasisi ya Masomo ya Kiarabu na Kiislam mjini Roma, PISAI. Kunako mwaka 2015 ameshiriki katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia baada ya kuchaguliwa kuwakilisha Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.