2016-02-17 10:51:00

Iweni ni mashuhuda wa sala inayomwilishwa katika maisha!


Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume nchini Mexico, Jumanne tarehe 16 Februari 2016 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Wakleri, Watawa na Majandokasisi waliofurika kama umande wa asubuhi kwenye Uwanja wa “Venusiano Carranza” huko Morelia kwa kukazia kwa namna ya pekee, maisha yanayojikita katika sala, ushuhuda wenye mvuto kwa watu ili kuweza kumwamini na kumtumainia Mwenyezi Mungu katika maisha.

Sala ni tendo ambalo watu wanajifunza kama vile wanavyojifunza kutembea, kuzungumza na kusikiliza. Sala ni shule ya maisha inayomwilishwa katika maisha, kielelezo cha imani tendaji kama anavyokaza kusema Mtakatifu Paulo katika Waraka wake kwa Tito. Waamini wanaendeleza maisha ya sala kutokana na kile walichojifunza kutoka kwenye familia zao na baadaye, wanaendelea kukua na kukomaa katika sala kama ilivyo pia katika maisha.

Yesu katika maisha na utume wake amewafunulia waje wake Fumbo la maisha yake wakati wa chakula na mapumziko;  wakati alipokuwa anaponya, anahubiri na kusali, kwa kuwaonesha jinsi ambavyo Mwana wa Mungu anapaswa kuwa. Akawafundisha kuingia na kuzama katika maisha na utume wake, kiasi hata cha kuwa na ujasiri wa kumuita Mwenyezi Mungu, “Baba Yetu”, kielelezo cha ladha na mang’amuzi thabiti ya maisha; kwa kusali ile Sala, Yesu aliimwilisha katika utume wake, mwaliko kwa waamini kutenda kama alivyofanya Yesu, kwa kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma ya upendo wa Mungu katika maisha na historia.

Wito wa kwanza anaoutoa Mwenyezi Mungu kwa waja wake anasema Baba Mtakatifu ni kuwaingiza waja wake katika mwelekeo mpya wa upendo, kwa kujifunza kumwita Mwenyezi Mungu, Abba, yaani Baba Yetu, tayari kutoka kifua mbele ili kuinjilisha si kwa ajili ya utukufu wa mtu, bali kwa kutambua kwamba, hii ni dhamana nyeti inayopaswa kutekelezwa. Ole wao wakleri, watawa na majandokasisi ikiwa kama watashindwa kuwa ni mashuhuda wa kile walichoona na kusikia.

Wao ni watendakazi katika shamba la Bwana, wanaoitwa na kushirikishwa maisha ya Mungu kwa njia ya sala inayomwilishwa katika matendo. Utume wao ni ushuhuda wa maisha na kamwe wasikubali kutumbukia katika vishawishi, hata Yesu mwenyewe alilitambua hili, akawaombea mitume wake. Hivi ni vishawishi vinavyojitokeza katika mazingira ya uhalifu, rushwa na ufisadi; biashara haramu ya dawa za kulevya; udhalilishaji wa utu na heshima ya binadamu; tabia ya kutojali mahangaiko na masumbuko ya wengine. Huu ni mfumo unoonekana kuwavuta wengi kwa ajili ya mafanikio na utukufu wa mtu binafsi!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika vishawishi na changamoto zote hizi, wakleri, watawa na majandokasisi kamwe wasikate tamaa na kukubali kushindwa na shetani kwa kutumia hali kama hii kama silaha yake madhubuti. Kukata na kujikatia tamaa kutawadumaza kiasi cha kushindwa kusonga mbele wala kuona njia ya maisha; watashindwa kutangaza, kusali na kupanga maisha yao kwa siku za usoni. Ndiyo maana Baba yao wa mbinguni hapendi kuwaona wanatumbukia katika vishawishi. Wawe na ujasiri wa kufanya kumbu kumbu ya historia katika maisha yao hadi hapo walipofikia.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu amemkumbuka Askofu Vasco Vàsquez de Quiroga, Askofu wa kwanza wa Jimbo hilo aliyejisadaka na kusimama kidete kulinda na kuwatetea wenyeji wa Chiapas; shida na mahangaiko aliyoyapata, zilikuwa ni malipizi ya dhambi zake kama Padre. Alisikitika kuona jinsi Wahindi Wekundu wakivyokuwa wanadhalilishwa na kunyanyaswa kana kwamba, walikuwa ni bidhaa za kuuzwa sokoni. Akaguswa na mahangaiko yao na akaanza kuweka mbinu mkakati wa kuwasaidia; akageuza sala kuwa ni sehemu ya maisha, kiasi kwamba, Wahindi wekundu wakamtambua kuwa Baba mwema, na kumpachika jina “Tata Vasco” maana yake, Baba Vasco!

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri yake kwa kusema, hii ndiyo sala ambayo Kristo Yesu amewafundisha wafuasi wake. Ni sala inayowaimarisha ili kamwe wasitumbukie katika vishawishi; kwa kukata na kujikatia tamaa ya maisha. Wawe na ujasiri wa kufanya kumbu kumbu ya historia ya maisha, kwa kuwaangalia wale waliowarithisha imani, ili waweze kuwa na ujasiri wa kusema, Baba Yetu! Baba Mtakatifu Francisko amemshukuru kwa namna ya pekee Kardinali Alberto Suàrez Inda, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Morelia kwa kumruhusu kutumia Fimbo ya Kiaskofu na Kalisi ya Hayati Askofu Vasco Vasquaez de Quiroga, Askofu wa kwanza wa Jimbo la Michoacan, mlinzi na mtetezi wa Wahindi wekundu, ayejulikana kama “Tata Vasco”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.