2016-02-16 10:02:00

Onesheni ujasiri wa kuomba msamaha!


Familia ya Mungu mjini Chiapas, nchini Mexico imempokea Baba Mtakatifu Francisko katika mji wao kwa bashasha na shangwe kubwa iliyokuwa inajionesha katika nyuso za watu, katika midundo na rangi za mavazi yao. Bahari ya watu ilifurika, siku ya Jumatatu tarehe 15 Februari 2016 huko Chiapasa, wakati Baba Mtakatifu alipokwenda mjini humo kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu pamoja na wenyeji wa Chiapas, huko San Cristobal, DLC. Ibada hii imeadhimishwa kwa kutumia lugha mahalia, changamoto ya kutamadunisha Injili ili kweli Injili iweze kuingia na kuzama katika maisha, mila na tamaduni za watu!

Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu anasema, Neno la Mungu linafanya rejea katika maisha ya watu wa Chiapas, ambao kwa miaka mingi walitengwa, wakadhulumiwa na kunyanyaswa na mifumo mbali mbali ya kisiasa. Umefika wakati wa kuchunguza dhamiri na kuomba msamaha kwa makosa yaliyotendeka katika historia, tayari kuanza kuandika ukurasa mpya unaojikita katika haki msingi za binadamu, sanjari na utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote! Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, Waisraeli walipokuwa utumwani Misri walionja mateso na nyanyaso, wakamlilia Mungu naye akawasikiliza, kwa kuwaonesha uso wa huruma kwa njia ya Neno na Sheria zake, ambazo zikawa ni chemchemi ya uhuru, furaha, hekima na mwanga wa maisha kwa watu waliokuwa wanatembea katika giza la maisha. Hata wananchi wa Chiapas anasema Baba Mtakatifu kwa miaka mingi wametembea katika dhuluma na nyanyaso; wakang’olewa hata katika ardhi yao; mambo ambayo yameacha chapa ya kudumu katika nyoyo za watu!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, umefika wakati wa kujenga na kudumisha udugu, haki, mshikamano na amani, kwa kutambua kwamba, haya ni mambo msingi yanayowaunganisha wote kama watoto wa Baba yao wa mbinguni, aliyewaletea Kristo Yesu, anayetembea pamoja nao katika hija yao ya maisha. Yesu ni njia, ukweli na uzima anayetaka kuwasaidia waja wake kushinda giza la maisha. Nyanyaso na dhuluma zimesababisha madhara makubwa katika maisha ya watu wengi, lakini bado Mwenyezi Mungu anaonesha huruma na upendo kwa waja wake.

Baba Mtakatifu anaendelea kukemea vikali matumizi mabaya ya rasilimali na utajiri wa dunia ambao ni zawadi kubwa kwa binadamu kwa kudhani kwamba, wao ni wamiliki na kusahau kuwa wamedhaminishwa na Mwenyezi Mungu ili kuitunza na kuiendeleza dunia, iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Vita inayojikita bado katika mioyo ya binadamu ni matokeo ya madhara ya dhambi yanayojionesha hata katika matumizi mabaya ya ardhi na maji pamoja na kusababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira; mambo ambayo yana athati kubwa katika maisha ya watu wengi.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, athari za uchafuzi wa mazingira zinawagusa binadamu wote na kwamba, hii ni kati ya changamoto kubwa inayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Wananchi wa Chiapas ni mfano bora wa kuigwa kwa kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kujifunza mengi kutoka kwao. Mazingira imekuwa ni nyumba ya wote, chanzo cha lishe na Altare ya ushirikiano kati ya watu!

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema, wananchi wa Chiapas wakati mwingine hawakueleweka; tunu msingi, tamaduni na mapokeo yao yakadhalilishwa; kwa watu kutaka kukumbatia madaraka, utajiri, fedha huku wakisukumwa na kanuni msingi za soko; wakawekeza katika mambo makubwa, ambayo kwa wakati huu ni chanzo kikuu cha uharibifu wa mazingira. Umefika wakati wa kuchunguza dhamiri na kuthubu kuomba msamaha kutokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengi kwa kuonesha kwamba, hata wao ni muhimu sana katika mchakato wa maendeleoya jamii.

Baba Mtakatifu anasema, vijana wa kizazi kipya wanakabiliwa na changamoto nyingi za maisha, wanapaswa kusaidiwa ili kulinda na kudumisha hekima kutoka kwa wazee wao, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya nchi yao. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema waendelee kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu aliyewaumba na kuwakomboa anaendelea kufanya hija ya maisha pamoja nao. Kwa njia ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, waamini wanaadhimisha: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.