2016-02-16 15:05:00

Kutoa taarifa kwa vyombo vya sheria ni wajibu wa kimaadili!


Kardinali Seàn O’Malley, Rais wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya ulinzi kwa watoto wadogo, kwa kushirikiana na wajumbe wote wa tume hiyo wanasema nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo hazipaswi kuwa tena masuala ya siri bali zinapaswa kutolewa taarifa kwa vyombo vya sheria ili haki iweze kutendeka kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko. Kanisa linapaswa kuwajibika kisheria sanjari na kulinda utu na heshima ya watoto dhidi ya nyanyaso kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya kisheria. Huu ni wajibu wa kimaadili.

Kardinali Seàn O’Malley anafafanua kwamba, nchini Marekani, inaeleweka wazi kwamba viongozi wa Kanisa wanawajibika kutoa taarifa kuhusiana na nyanyaso za kijinsia kwa watoto wadogo kwa vyombo vya sheria. Kila mwaka Maaskofu wanapokutana, agizo hili linatiliwa mkazo zaidi na kwamba, Maaskofu wapya wanaendelea kupewa mafunzo kuhusiana na changamoto hii katika maisha na utume wa Kanisa. Tume hii ya Kipapa hivi karibuni imemshirikisha Baba Mtakatifu sera na mikakati iliyofanyiwa kazi kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita na kwamba, kozi hii itatolewa pia mjini Roma kwa ajili ya Maaskofu wapya na maafisa waandamizi wa Sekretarieti kuu ya Vatican, ili waweze kuutumia ujuzi huu katika utekelezaji  wa majukumu yao ya kila siku ili kuwalinda na kuwatetea watoto wadogo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.