2016-02-16 14:31:00

Baba Mtakatifu anasali na anataka kuwafariji wote!


Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican anasema, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 15 Februari 2016 akiwa nchini Mexico ametembelea Kanisa kuu la San Cristòbal de las Casas, mahali ambapo Askofu Samuel Ruiz amefundisha, akaongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa kipindi cha miaka 40 na hatimaye, akazikwa ndani mwake. Akiwa Kanisani hapo amekutana na kuzungumza na umati mkubwa wa waamini na kusali kwa kitambo kidogo.

Askofu Samuel Ruiz alitoa kipaumbele cha kwanza kwa shughuli za kichungaji miongoni mwa wenyeji wa Chiapas, ambamo leo hii kuna kundi kubwa la Mashemasi wa kudumu, wenye familia na watoto; ambao wamekuwa mstari wa mbele katika Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima. Hawa ni mashuhuda wa Neno la Mungu, Liturujia na maisha ya waamini katika Jumuiya za Kikristo.

Baba Mtakatifu alipata pia nafasi ya kushiriki chakula cha mchana na wenyeji wa Chiapas, kama anavyofanya wakati wa hija zake za kitume kwa kutembelea wakimbizi, wafungwa, wagonjwa na maskini, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu kwa kutambua kwamba, wao ni kiini cha Injili ya Kristo. Wawakilishi wa Familia ya Mungu nchini Mexico wameshiriki chakula cha mchana na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na kuzungumza nao!

Maandalizi ya Ibada ya Misa Takatifu huko Ciudad Juàrez, Jumatano tarehe 17 Februari 2016. Hili ni eneo ambalo lina utata mkubwa kwani inakadiriwa kwamba, zaidi ya watu 27, 000 wamepotea eneo hili katika mazingira ya kutatanisha katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha uwepo wa karibu kwa wote walioguswa na kutikiswa na matukio haya, ili aweze kuwaimarisha katika maisha yao, tayari kusonga mbele kwa matumaini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.