2016-02-15 11:48:00

Iweni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu!


Mpendwa Msikilizaji wa Kipindi cha Hazina yetu, Tunakusalimu kutoka katika Studio za Radio Vatikan tukisema Tumsifu Yesu Kristo. Tumo katika kipindi cha Kwaresma; siku arobaini tunazojaaliwa na Mama Kanisa Mtakatifu: katika mwendo wa Liturujia ya Mwaka, ili tuweze kushughulikia wongofu wetu sisi wenyewe. Kwaresma ni kipindi cha kutafakari juu ya thamani yetu kama watu tulioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Ni kipindi cha kujichunguza kama kweli hali zetu zinaakisi ule uzuri ambao Mungu aliuweka ndani mwetu. Kwaresma ni kipindi cha kumshukuru Mungu zaidi kwa kutuumba, kwa sura na mfano wake, mwaliko wa kujibidisha kuutunza ule uzuri ambao Mungu mwenyewe ameuweka ndani mwetu. Na kwa pale ambapo tumeukwaruzakwaruza ule uzuri aliouweka Mungu ndani mwetu; basi, Kwaresma ni kipindi cha kuvaa ujasiri kujinyooshea kidole sisi wenyewe katika mapungufu yetu, kujiambia ukweli wa ndani ili tuweze kufanya mabadiliko ya kweli.

Tukijihukumu katika ukweli, tutagundua kwamba hapa na pale hatukuenenda kwa usahihi sana. Basi,  Kwaresma ni kipindi maalumu cha kurekebisha makunyanzi, kuondoa tofauti, kufanya toba ya kweli na kuanza upya katika Kristo. Ni kipindi ambacho tunaalikwa kuuachilia utu wa kale (yaani dhambi) na kuuvaa utu mpya, (yaani uungwana na utakatifu wa Mungu).

Mpendwa msikilizaji, tunaiishi Kwaresma yetu tukiwa ndani ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu; mwaka mtakatifu ambapo sisi sote tumealikwa kutafakari na kuishukuru sana huruma ya Mungu wetu; ambayo wakati mwingine tunaipokea bila hata kujua. Moja ya sehemu ya Huruma ya Mungu, ni uvumilivu wake kwetu na msamaha anaotujaalia pale tunapokuwa tumekosea. Bwana Mungu; ni Baba mwenye Huruma, asiye penda dhambi lakini hamchukii mdhambi, bali anatualika sote tutubu, tuongoke: maana hapendi mtu yoyote apotee bali wote watubu (rej. 2Pet. 3:9-13).

Kumbe, kipindi hiki cha Kwaresma ni kipindi cha kuomba zaidi na zaidi huruma ya Mungu. Sio kwa ajili yetu tu, bali kwa ajili ya wengine pia. Tunaalikwa sote kuwa wafadhili wa huruma ya Mungu. Tuwaonjeshe na jirani zetu, marafiki zetu na hata wale wasiotutakia mema huruma na wema wa Mungu; kwani Mwanadamu kisha guswa na huruma ya Mungu, huweza kufanya mabadiliko makubwa sana katika maisha; na akawa mtu wa pekee na mwenye kufaa zaidi katika jamii ya watu. Ndivyo ilivyokuwa hata kwa Matayo Mtoza ushuru (rej. Mt. 9:9-13), Mt. Mtume Paulo na watakatifu wengine wengi sana.

Ndivyo hata katika nyakati zetu, mtu awaye yoyote akionjeshwa Huruma ya Mungu, huruma hiyo ya Mungu hufanya makuu. Ni huruma yenye kumbadilisha mtu kutoka katika undani wa nafsi yake. Ni huruma ambayo hufungua mlango wa matumaini. Ni huruma ambayo huthibitisha upendo-jamii, ambao ni kiu ya kila mwanadamu; yaani kujisikia kuwa anapendwa na jamii inayomzunguka, anathaminiwa na anapokelewa.

Tumesikia mengi na mara nyingi juu ya neno hili “huruma”. Na Maandiko Matakatifu yanampa heri mtu mwenye huruma kwani naye pia atahurumiwa (rej. Mt. 5:7). Na sisi katika maisha yetu ya kila siku, sio mara moja tumewahi kutamka neno hili huruma au nihurumie! Tulieleweje basi neno hili? Pamoja na tafanusi nyingine nyingi sana tunazozifahamu juu ya neno huruma;  kwa kipindi hiki cha Kwaresma, tuone kwa ufupi neno huruma lataka kutuambia nini au mtu anapoomba huruma anataka kusema nini.

Huruma ni neno linaloalika, msaada. Mtu akisema tafadhali nihurumie, huenda anaomba msaada asaidiwe katika jambo gumu linalomtatiza. Ni neno pia lenye kualika msamaha, kwa makosa tuliyotenda. Kuomba huruma ni kuomba tusipatilizwe kwa makosa yetu lakini huku tukiwa na kite cha roho cha kuwa tayari kurekebisha makosa yetu. Huruma ni neno linaloalika upendo na wema kutoka kwa wenzetu. Ni neno pia linaloakisi Haki, Uaminifu, Roho njema, Upendo, Maelewano mema na Amani.

Hivyo tunapoalikwa kuwa watu wenye huruma kama Baba yetu wa Mbinguni; kwa mantiki halisi tunaalikwa kuwa watu wenye waki, waaminifu, tusiwe na roho mbaya kwa wenzetu, tujawe na upendo, tuwe watu wenye kukuza maelewano mema kati ya watu na mwisho tuweze kujenga amani ya kweli kati yetu. Mahali penye watu wenye huruma, daima patafurika wingi wa amani; kwa sababu mtu yoyote mwenye tunu ya kupenda huruma, kamwe hafurahi udhalimu, hafurahii roho mbaya wala magombano, bali daima hupenda kujenga ile amani binafsi rohoni na amani katika jamii.

Hivyo mpendwa msikilizaji, katika kipindi hiki cha kwaresma, yote ambayo tunapaswa kutenda kadiri ya Desturi za Dini yetu Takatifu sana Katoliki; yanatuelekeza kuitambua, kuikimbilia, kuiambata na kuiishi huruma ya Mungu, bila kusahau kuwafadhilia wengine huruma ya Mungu.

Tusikilizane tena kipindi kijacho, nikikutakia kila la heri na baraka kwa kipindi cha Mfungo wa Kwaresima; kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.