2016-02-15 10:39:00

Changamoto za utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!


Utu, heshima na utamaduni wa watu mahalia unapaswa kulindwa, kutunzwa na kudumishwa kwani kutokana na changamoto za maendeleo katika ulimwengu wa utandawazi, watu hawa na tunu zao msingi wanaweza kujikuta wametelekezwa na hatimaye kung’olewa katika maeneo na makazi yao; hali inayodhalilisha utu wa binadamu. Wenyeji wa Mexico ni ushuhuda makini kwa Jumuiya ya Kimataifa kwamba, binadamu anaweza kuishi vyema, huku akitunza na kuendeleza mazingira, nyumba ya wote.

Huu ni ujumbe kutoka kwa Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani kwa wajumbe wanaoshiriki kongamano kuhusu Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, Laudato si, unaofanyika kati ya tarehe 13- 14 Februari 2016 huko San Cristo’bal de Las Casas mjini Chiapas. Wenyeji wameonesha mwanga angavu katika mchakato wa kuleta mabadiliko kwa kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Haya ni maandalizi yanayofanywa na wenyeji ili kumpokea na kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko huko Chapas, tarehe 15 Februari 2016. Baba Mtakatifu anataka kukutana na kuzungumza na wenyeji wa Chiapas ili kuwatia shime katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Binadamu wa nyakati hizi anasema Kardinali Turkson anaishi katika ulimwengu wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine kwa kujikita katika dhana ya teknolojia. Mara nyingi watu wanashuhudia uvunjwaji wa haki msingi za binadamu na zile za kijamii, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na mwelekeo mpya na chanya kwa kuiga mambo mazuri kutoka kwenye Jumuiya za wenyeji ili kulinda na kutunza mazingira badala ya kumezwa na malimwengu kwa kujikita katika kutafuta fedha na utajiri wa haraka haraka bila kuzingatia utu na heshima ya binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira.

Kardinali Turkson anakaza kusema, maskini wamejipanga vyema katika kupambana na utamaduni wa ubaguzi, kashfa ya ukosefu wa haki na usawa wa kijamii pamoja na uharibifu mkubwa wa mazingira, nyumba ya wote. Matokeo yake, makundi haya ya kijamii yameanzisha mtandao wa kijamii si tu kwa ajili ya kupambana na ukosefu wa haki msingi za binadamu katika jamii, bali pia kupata ufumbuzi wa matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo kwa kukosa makazi bora, ardhi kwa shughuli zao pamoja na fursa za kazi kwa kutambua kwamba, kazi ni utambulisho na utilimifu wa utu na heshima ya binadamu.

Hizi ni changamoto ambazo Serikali na soko huria zimeshindwa kuzipatia ufumbuzi wa kudumu. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwatia shime maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kushikamana kwa dhati kwa ajili ya mustakabali wa maendeleo yao pamoja na kuonesha nguvu ya umoja ambayo kimsingi ni silaha madhubuti kwa wanyonge. Licha ya magumu na changamoto wanazokabiliana nazo wenyeji wengi ndio wakulima wanaozalisha mazao ya chakula; ni wajenzi na watengnenezaji wa fursa za ajira kwa watu wengi zaidi. Mama Kanisa anapenda kushiriki kikamilifu katika mchakato huu wa mageuzi kwa kutoa mchango wake ili vyama vya ushirika na makundi ya kijamii yaweze kushikamana ili kukabiliana na changamoto za maisha kadiri ya uwezo uliopo, ili kuwa ni sehemu ya maendeleo ya Jumuiya ya Kimataifa, vinginevyo watajikuta wamebaki nyuma na kubaguliwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.