2016-02-13 09:28:00

Tamko la pamoja kati ya Papa Francisko na Patriaki Kirill wa Moscow


Neema ya Bwana Yesu Kristo, na pendo la Mungu, na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote! Kwa utashi wa Mwenyezi Mungu asili ya kila zawadi, katika jina la Yesu Kristo na kwa njia ya msaada wa Roho Mtakatifu Mfariji, Papa Francisko na Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima, waliokutana mjini Havana, Cuba, tarehe 12 Februari 2016 wanamshukuru Mwenyezi Mungu na kulitukuza Fumbo la Utatu Mtakatifu kwa kufanikisha tukio hili la kihistoria, kwa kuwawezesha viongozi hawa wakuu kukutana kwa mara ya kwanza katika historia na hatimaye kutoa tamko la pamoja kati ya viongozi hawa wakuu wa Kanisa Katoliki la Kanisa la Kiorthodox.

Kwa pamoja wanasema, wamekutanika kwa furaha kama ndugu wamoja katika imani ya Kikristo ili kuzungumza ana kwa ana; moyo kwa moyo na kujadili mahusiano ya Makanisa haya mawili, matatizo na changamoto msingi za waamini wao na matumaini katika ustawi na maendeleo ya ustaarabu wa binadamu. Mkutano huu umefanyika nchini Cuba, mahali pa makutano kati ya Kaskazini na Kusini; Mashariki na Magharibi. Cuba ni kielelezo cha matumaini ya “Dunia mpya” na matukio ya kusikitisha yaliyojitokeza katika Karne ya XX. Viongozi wakuu wa Makanisa haya mawili wanasema, Tamko hili liifikie Familia ya Mungu mahali popote pale ilipo!

Viongozi hawa wanafurahi kuona kwamba, imani ya Kikristo inaendelea kukua na kushamiri. Amerika ya Kusini inaonesha nguvu ya maisha ya kiroho inayojikita katika Mapokeo ya Kikristo yaliyowezeshwa kutokana na mang’amuzi ya mamillioni ya watu; uhakika wa maendeleo makubwa ya kiroho kwa Amerika ya Kusini kwa siku za usoni. Viongozi hawa wameamua kukutana mbali kabisa na mitafaruku “Bara la Ulaya” na kwamba, wanajisikia kuwa na nguvu inayowasukuma Wakatoliki na Waorthodox kushirikiana kwa unyenyekevu na heshima ili kushuhudia kwa ulimwengu tumaini lililomo ndani mwao. Wanamshukru Mwenyezi Mungu kwa ujio wa Mwanaye Mpendwa anayewawezesha kushirikishana  Mapokeo ya maisha ya kiroho yanayobubujika kutoka katika karne ya kwanza ya Ukristo. Mashuhuda wa Mapokeo haya ni Bikira Maria, Mama wa Mungu na Watakatifu wanaowaheshimu pamoja na mashuhuda wa imani walionesha uaminifu wao kwa Kristo kiasi cha kuwa ni “mbegu ya Ukristo”.

Licha ya Mapokeo haya ya pamoja kati ya Wakatoliki na Waorthodox, katika karne kumi zilizopita wameshindwa kuonesha umoja katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Wametengana kutokana na madonda yaliyosababishwa na mipasuko kwa nyakati mbali mbali; wakapoteza urithi waliopokea kutoka kwa Mababu wa imani kuhusu Imani kwa Mungu mmoja mwenye Nafsi tatu: Yaani: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Utengano hii ni matokeo ya mapungufu ya kibinadamu na dhambi licha ya Sala ya Kikuhani iliyotolewa na Kristo Mkombozi “Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu, ili ulimwengu upate kusadiki” Yoh. 17: 21.

Viongozi hawa wanatambua kwamba, kuna vikwazo, lakini ni matumaini yao kuwa mkutano huu utasaidia kuvuka vikwazo vya kihistoria vinavyoendelea kukwamisha umoja kadiri ya matakwa ya Mungu, jambo ambalo Kristo mwenyewe alisali na kuliombea. Mkutano huu uwahamasishe Wakristo sehemu mbali mbali za dunia ili kusali na kumwomba Kristo Bwana kwa ari na moyo mkuu ili aweze kuwajalia  wafuasi wake umoja kwa kutambua kwamba, ulimwengu unatarajia si tu kusikia maneno bali matendo kamili; mkutano huu uwe ni alama ya matumaini kwa watu wote wenye mapenzi mema.

Viongozi hawa wanadhamiria kutekeleza kile kinachowezekana ili kuvuka vikwazo walivyorithi katika historia kwa kuunganisha nguvu zao ili kushuhudia Injili ya Kristo kwa pamoja, amana ya Kanisa katika Millenia ya kwanza ya Ukristo, kwa kujibu kwa pamoja changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo. Wakatoliki na Waorthodox wanapaswa kujifunza kutoa ushuhuda wa ukweli mahali pa lazima na pale inapowezekana. Ustaarabu wa mwanadamu umeingia katika mageuzi makubwa. Dhamiri yao ya Kikristo na wajibu wao wa kichungaji unawahimiza kusimama kidete ili kuweza kukabiliana na changamoto hizi zinazohitaji jibu la pamoja! Viongozi hawa wanapenda kuyaelekeza mawazo yao katika maeneo ambamo Wakristo wanaendelea kuteswa na kunyanyaswa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Hawa ni wale wanaoishi huko Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini, huko Wakristo wanauwawa kikatiliki; Makanisa yao yameharibiwa na kufanyiwa kufuru; Makumbusho yao yameharibiwa vibaya.

Huko Syria, Iraq na katika baadhi ya Nchi zilizoko Mashariki ya Kati, kuna makundi makubwa ya Wakristo wanaolazimika kukimbia maeneo ambayo yalikuwa ni chemchemi ya imani ya Kikristo, waliyoimwilisha katika maisha yao tangu nyakati za Mitume, huku wakiishi kwa amani na wamini wa Jumuiya za dini nyingine. Viongozi hawa wanaitaka Jumuiya ya Kimataifa kutekeleza haraka inavyowezekana kuzuia Wakristo kufukuzwa huko Mashariki ya Kati. Wanapenda kupaaza sauti zao ili kuwatetea Wakristo wanaonyanyaswa na kudhulumiwa; wanapenda kuwafariji pia waamini wa dini nyingine wanaoteseka kuwa ni sehemu ya wahanga wa vita ya wenyewe kwa wenyewe pamoja na vitendo vya kigaidi.

Vita nchini Syria na Iraq vimekwisha sababisha athari kubwa kwa watu na mali zao na hivyo kusababisha mamillioni ya watu kukosa makazi na rasilimali. Makanisa yanawaomba viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuungana kwa pamoja ili kukomesha vita na vitendo vya kigaidi wakati huo huo isaidie kuchangia katika mchakato wa majadiliano ili amani iweze kupatikana haraka iwezekanavyo. Waathirika wawe na fursa ya kupata msaada wa kiutu bila kuwasahau wakimbizi na wahamiaji walioko kwenye nchi jirani. Viongozi wa Makanisa wanawasihi wale wote wanaoweza kuchangia kwa namna moja au nyingine kusaidia kuachiliwa huru watu waliotekwa nyara, kati yao wakiwa ni Maaskofu wakuu wa Aleppo, Paolo na Giovanni Ibrahim waliotekwa nyara mwezi Aprili 2013. Wanaendelea kupaaza sauti zao kwa ajili ya kuombea amani huko Mashariki ya kati, ili kweli amani hii iweze kuwa ni matunda ya haki yatakayosaidia watu kuishi kwa pamoja kama ndugu; wakimbizi waweze kupata fursa ya kurejea tena makwao; waliojeruhiwa waweze kuganga na kuponywa majeraha yao na roho za marehemu waliouwawa kikatili ziweze kupata pumziko la amani.

Viongozi wa Makanisa wanawaomba wadau mbali mbali wanaohusika na vita waoneshe utashi wa kisiasa kwa kukaa pamoja katika meza ya majadiliano. Wakati huo huo, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba inasitisha vitendo vyote vya kigaidi kwa kuwa na sera na mipango inayoratibiwa kwa umoja. Wanaziomba nchi zote ambazo zinaendelea kupambana na vitendo vya kigaidi, kuendelea kutekeleza dhamana hii kwa kuwajibika na kwa busara. Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kusali ili kumwomba Mwenyezi Mungu kulinda viumbe vyake dhidi ya uharibifu na kamwe asiruhusu Vita kuu ya Tatu ya Dunia kutokea. Ili watu waweze kuwa na amani ya kudumu kuna haja ya kusaidia mchakato wa watu kugundua tunu msingi zinazowaunganisha; tunu ambazo zinapata msingi wake kutoka katika Injili ya Kristo Yesu.

Wanapiga magoti mbele ya mashuhuda wa imani walioyamimina maisha yao ili kushuhudia ukweli wa Injili; wakathubutu kukubali kifo badala ya kuikana imani yao kwa Kristo. Mashuhuda wa imani kutoka katika Makanisa mbali mbali, waliounganishwa kwa mateso makali ni chachu muhimu sana ya Umoja wa Wakristo. Wanapenda kuwapongeza kwa kuwa wanashiriki katika mateso ya Kristo. Kutokana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo, majadiliano ya kidini ni jambo muhimu sana. Uelewa tofauti wa kweli za kidini kisiwe ni kisingizio kwa waamini wa dini mbali mbali kutoishi kwa amani na utulivu. Katika mazingira haya, viongozi wa kidini wanayo dhamana kubwa ya kuwafunda waamini wao ili waweze kuwa na moyo wa kuheshimu waamini wa dini na Mapokeo mengine ya kidini. Ni jambo ambalo halikubaliki hata kidogo kutumia dini kwa ajili ya kuhalisha mauaji kwani Mwenyezi Mungu si Mungu wa vita bali ni Mungu wa amani.

Viongozi wa Makanisa wanapenda kukazia uhuru wa kuabudu kwa kumshukuru Mungu kwa mchakato wa upyaisho wa imani ya Kikristo unaoendelea kujitokeza nchini Russia kwa wakati huu na katika Nchi nyingi za Ulaya ya Mashariki; maeneo ambayo yalitawaliwa kwa Serikali za mabavu. Leo hii Wakristo wengi wanaweza kushuhudia imani yao; kumekuwepo na ujenzi wa Makanisa; Nyumba za Kitawa na Taasisi za Kitaalimungu. Wakristo wanaendelea kuchangia kwa hali na mali katika huduma ya upendo kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini wa Makanisa haya mawili wamekuwa wakishirikiana bega kwa bega, ushuhuda wa hazina ya maisha yao ya kiroho, utu na tunu msingi za Kiinjili.

Hata hivyo, kuna baadhi ya nchi ambazo uhuru wa kuabudu na haki ya kushuhudia na kumwilisha imani hiyo katika uhalisia wa maisha, unakumbana na makwazo, kiasi hata kutaka kung’oa aina yoyote ile ya rejea kwa Mwenyezi Mungu pamoja na ukweli wake; mambo ambayo kimsingi ni hatari sana kwa uhuru wa kuabudu. Wakristo wanaendelea kubanwa na wakati mwingine kunyimwa haki zao msingi kutokana na sera na mikakati ya kisiasa ambayo wakati mwingine ina mielekeo hasi ya kutaka kulisukumizwa Kanisa pembezoni mwa maisha ya hadhara.

Mchakato wa ujenzi wa Bara la Ulaya baada ya miaka mingi ya vita na kinzani, ulipokelewa kwa matumaini kwa kuamini kwamba, ungechangia kwa kiasi kikubwa kustawisha amani na utulivu. Lakini, ujenzi wa Ulaya usiozingatia utambulisho wa kidini ni hatari kwani dini zimechangia kwa kiasi kikubwa ustawi na maendeleo ya watu, mwaliko kwa Bara la Ulaya kuwa aminifu kwa misingi yake ya Kikristo. Wakristo wanapaswa kutoka kifua mbele ili kumshuhudia Kristo na Injili yake, ili kudumisha Ulaya ambayo imejengwa katika Mapokeo ya Kikristo, takribani Millenia mbili zilizopita. Viongozi wa Makanisa katika Tamko lao la pamoja wanaangalia umaskini unaoendelea kuwadhalilisha watu wengi, ingawa kuna ongezeko la utajiri mkubwa wa vitu. Kuna mamillioni ya wakimbizi na wahamiaji wanaobisha hodi katika malango ya nchi tajiri duniani. Kuna ulaji wa kutisha katika baadhi ya nchi tajiri, hali inayomeng’enyua utajiri wa dunia hii pamoja na mipasuko ya kijamii inayotokana na ugawaji mbaya wa rasilimali na utajiri wa dunia. Yote haya yanachangia ongezeko la ukosefu wa haki katika mfumo wa mahusiano ya kimataifa.

Wakristo wanaalikwa kusimama kidete kulinda na kutetea haki, kuheshimu tamaduni za watu na kushikamana na wote wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia. Familia ni kiini cha maisha ya mwanadamu na jamii katika ujumla wake. Mmong’onyoko wa tunu bora na misingi ya kifamilia ni mambo yanayoleta mashaka na wasi wasi mkubwa sehemu mbali mbali za dunia. Wakristo wanahamasishwa kushikamana na kushuhudia tunu bora za kifamilia kama safari ya kuendea utakatifu wa maisha; kwa kuonesha ushuhuda wa wanandoa katika mahusiano yao; tayari kupokea  watoto ambao ni zawadi kutoka kwa Mungu na kuwalea. Wakristo waoneshe mshikamano kati ya kizazi kimoja hadi kingine, kwa kuwaheshimu na kuwathamini wanyonge zaidi.

Familia inajikita katika msingi wa ndoa, tendo ambalo ni huru na aminifu katika mapendo kati ya bwana na bibi; upendo unafunga umoja na hivyo wanalazimika kupokeana kama zawadi. Ndoa ni shule ya upendo na uaminifu na kwamba, mifumo mingine nje ya ndoa ni kinyume cha mapenzi ya Mungu kwa mwanadamu kwani ubaba na umama ni wito mtakatifu kati ya bwana na bibi katika maisha ya ndoa yaliyobarikiwa na Mapokeo ya Kibiblia na kuwekwa katika maisha ya hadhara. Watu wote wanapaswa kuheshimu na kutunza zawadi ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba. Ikumbukwe kwamba, damu ya watoto hawa wachanga inamlilia Mungu. Kifo laini na maendeleo ya sayansi yanayotaka kuchezea maisha ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ni hatari sana. Kanuni maadili, utu na heshima ya binadamu zinapaswa kuzingatiwa na wote kadiri ya mpango wa Mungu.

Viongozi wa Makanisa wanawaalika vijana kutoka kimasomaso ili kuonesha karama na vipaji vyao na kamwe wasithubutu kuvizika ardhini, bali wawe tayari kuvitumia ili kuimarisha ukweli wa Kristo sanjari na kumwilisha ndani mwao amri ya upendo kwa Mungu na jirani; wawe makini kusimama kidete kulinda ukweli wa Mungu; wajitahidi kuwa kweli ni mwanga na chumvi ya dunia kwa njia ya ushuhuda wa matendo yao mema yenye mvuto na mashiko. Wazazi wanaalikwa kuwarithisha na kuwaelimisha watoto wao misingi ya imani, kwani wamekombolewa kwa Damu Azizi ya Kristo Yesu.

Wakatoliki na Waorthodox licha ya kuwa na Mapokeo ya pamoja, lakini pia wana utume unaowataka kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo katika ulimwengu mamboleo; kwa kujifunza kuishi kwa umoja, amani na maelewano; kwa kuheshimu uhuru wa waamini bila kulazimisha wongofu wa waamini wa Makanisa mengine; kwani kwa kufanya hivi ni kuharibu uhuru wa kidini na Mapokeo ya waamini hawa. Umefika wakati kwa waamini wa Makanisa haya mawili kuanza pia mchakato wa upatanisho ili kuondokana na kashfa za kinzani na utengano kati ya Makanisa. Juhudi za makusudi zifanyike ili kutosheleza mahitaji ya kiroho ya waamini wa Makanisa haya.

Viongozi hawa katika Tamko lao wanasikitika kusema kwamba, vita na machafuko ya kisiasa nchini Ukraine yamekwisha sababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao na kwamba, mambo haya yanaendelea kuchangia kuporomoka kwa uchumi na shughuli za kibinadamu. Wadau mbali mbali wanaohusika na mgogoro wa kivita nchini Ukraine wanaalikwa kuonesha hekima, mshikamano wa kijamii ili kuchukua hatua zitakazosaidia ujenzi wa amani. Jumuiya za Kikristo huko Ukraine zishiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya amani na utulivu; umoja na mshikamano wa kidugu.

Kwa namna ya pekee, Wakristo wanahamasishwa kushirikiana kidugu ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kwa kujikita katika kanuni maadili na uhuru wa kweli, ili dunia iweze kuona na kuamini. Wakristo wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kiroho kama  watu binafsi na jamii; ili kushuhudia ukweli wa Roho Mtakatifu katika uhalisia wa maisha ya watu kwa kutambua kwamba, Yesu Kristo Mkombozi anawategemeza na kuwaimarisha kiroho. Kristo ni chemchemi ya furaha na matumaini na kwamba, imani kutoka kwake ikimwilishwa, maisha ya binadamu yanapata maana mpya, kwani wote wanafumbatwa na huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima wanahitimisha Tamko lao la pamoja lililotiwa sahihi huko Havana, Cuba, tarehe 12 Februari 2016 kwa kuonesha matumaini yao kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu, kwa kukimbilia ulinzi na tunza yake ya kimama; ili kwa sala na maombezi yake awaimarishe katika udugu wale wote wanaomheshimu, ili waweze kuungana tena kadiri ya mapenzi ya Mungu kwa wakati muafaka; wadumu katika amani na maridhiano kama Watu wa Mungu kwa ajili ya utukufu wa Utatu Mtakatifu usiogawanyika kamwe!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.