2016-02-13 15:12:00

Baba Mtakatifu aonesha furaha ya ndani kwa kukutana na Patriaki Kirill!


Mara baada ya Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima kutia sahihi Tamko la Kichungaji, tarehe 12 Februari 2016 walipata nafasi ya kuzungumza na mashuhuda pamoja na waandishi wa bahari ili kuelezea furaha yao. Baba Mtakatifu anasema, katika mazungumzo yao ya faragha wamezungumza kama ndugu katika imani inayobubujika kutoka kwenye Kisima cha Ubatizo na kwamba, wamewekwa wakfu kama Maaskofu. Wamezungumza kuhusu Makanisa yao mawili na kukubaliana kimsingi kwamba, majadiliano ya kiekumene hayana budi kujikita katika hija ya pamoja.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, mazungumzo kati yao, yamefanyika katika udugu, ukweli na uwazi bila kupindisha maneno, kiasi kwamba, amejisikia faraja kubwa kutoka kwa Roho Mtakatifu wakati wote wa mazungumzo yao. Kwa namna ya pekee, anamshukuru na kumpongeza Patriaki Kirill kwa unyenyekevu, udugu na matumaini yake kwa ajili ya umoja wa Kanisa. Kwa pamoja wamepanga mambo ambayo yanapaswa kutekelezwa na Makanisa haya mawili kama kielelezo cha hija ya majadiliano ya kiekumene.

Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wadau mbali mbali walioshiriki katika kuandaa na hatimaye kufanikisha tukio hili la kihistoria. Amemshukuru na kumpongeza Rais Raul Castro wa Cuba. Kwa hatua hii muhimu, Cuba inaweza kuwa kweli ni nchi ya umoja, ili yote haya yawe ni kwa ajili ya sifa na utukufu wa Fumbo la Utatu Mtakatifu sanjari na ustawi wa Watu wa Mungu, chini ya usimamizi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu.

Kwa upande wake Patriaki Kirill amesema kwamba, mazungumzo yao yamejikita katika uhuru, ukweli na uwajibikaji kwa ajili ya Makanisa haya mawili sanjari na ustawi wa waamini wao. Ni mazungumzo ambayo yamekuwa na utajiri mkubwa kwani yamegusa hali halisi ya maisha ya watu wa nyakati hizi katika ulimwengu mamboleo. Wameonesha umuhimu wa kushirikiana na kushikamana kama Wakristo ili kushuhudia na kutangaza imani yao kwa Kristo Yesu. Wamegusia athari za vita na madhulumu; umuhimu wa kuheshimu zawadi ya maisha; kanuni maadili na utu wema; familia na jamii pamoja na umuhimu wa Makanisa kushiriki katika maisha ya hadhara pamoja na kumwomba Yesu Kristo awaimarishe katika nia yao njema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.