2016-02-12 13:41:00

Papa Francisko achonga na waandishi wa habari!


Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican, wakati wa hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Cuba na Mexico, Ijumaa tarehe 12 Februari 2016, kwa niaba ya waandishi wa habari 76 walioko kwenye msafara wa Baba Mtakatifu, amemtakia heri na mafanikio mema katika hija hii ya kihistoria. Kundi kubwa la waandishi wa habari ni wale wanaotoka Mexico ambao wamepewa upendeleo wa pekee ili kuhakikisha kwamba, ujumbe wa Baba Mtakatifu unawafikia walengwa.

Baba Mtakatifu amewashukuru waandishi wa habari kwa kazi kubwa wanayoifanya hasa kwa kuzingatia kuwa hija hii ni ndefu na ya kihistoria, kwani anapenda kukutana na kuzungumza na ndugu yake Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima. Anapenda kwenda kusali na kumsalimia Bikira Maria wa Guadalupe, ili kushangaa Fumbo la upendo wa Mungu linalofumbatwa katika maisha ya wengi.

Baba Mtakatifu amechukua nafasi hii kwa namna ya pekee kumshukuru Dr. Albeto Gasbarri ambaye kwa muda wa miaka 47 amejisadaka kwa kazi na utume mbali mbali mjini Vatican. Kwa muda wa miaka 37 ameratibu hija za kitume za viongozi wakuu wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Tangu wakati huu, Monsinyo Mauricio Rueda atakuwa mratibu mpya wa hija za kitume za viongozi wa Kanisa mjini Vatican. Dr. Gasbarri anatarajiwa kung’atuka rasmi kutoka katika uongozi hapo tarehe 29 Februari 2016.

Waandishi wa habari kutoka Mexico wamemzawadia Baba Mtakatifu kofia ya kitamaduni kutoka Mexico kama walivyofanya kwa Mtakatifu Yohane Paulo II miaka 37 iliyopita na kwa Papa Mstaafu Benedikto XVI na sasa kwa Baba Mtakatifu Francisko. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwatakia wote kazi na utume mwema wakati huu wa hija yake ya kitume nchini Mexico.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.