2016-02-12 14:12:00

Panapo majaliwa, Papa Francisko kutembelea Colombia 2017


Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 12 Februari 2016 akiwa njiani kuelekea Mexico kwa kupitia Cuba amesema kwamba, ikiwa kama majadiliano ya amani yanayoendelea nchini Cuba yatafikia muafaka, kunako mwaka 2017 atafanya hija ya kitume nchini Colombia, ili kuwaimarisha ndugu zake katika mchakato wa ujenzi wa haki, amani, upendo, huruma na mshikamano wa dhati. Baba Mtakatifu ameyasema haya wakati alipokuwa anajibu swali kutoka kwa mwandishi wa habari wa Colombia ambaye yuko kwenye msafara wa Baba Mtakatifu Francisko nchini Mexico.

Itakumbukwa kwamba, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, tarehe 20 Septemba 2015 akiwa nchini Cuba, aliwawakumbuka wananchi wa Colombia ambao kwa miaka mingi wamekabiliana na hali ngumu ya maisha kutokana na mapigano yanayoendelea nchini humo na kwamba, alikuwa anawaomba wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanajitoa mhanga ili kujenga na kudumisha amani na usalama kati ya wananchi wa Colombia.

Baba Mtakatifu alipenda kuunganisha damu ya watu wasiokuwa na hatia ambayo imemwagika kwa miaka mingi nchini Colombia kutokana na vita, iweze kuunganishwa na Damu Azizi ya Kristo Yesu pale juu Msalabani, ili kusitisha vita na kuanza mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi; haki na amani, ili hatimaye, umoja wa kitaifa na upatanisho viweze tena kutawala katika akili na mioyo ya watu. Kwa njia ya utashi wa wananchi wote wa Colombia inawezekana kwamba, iko siku haki, amani, umoja na udugu vitatawala; kwa kuheshimu taasisi za ulinzi na usalama; sheria za nchi na zile za kimataifa pamoja na Katiba ya nchi ambayo kimsingi ni sheria mama. Baba Mtakatifu aliwataka wananchi wote wa Colombia kujifunga kibwebwe ili kwamba, mchakato wa majadiliano yaliyoanzishwa uzae matunda ya haki, amani na upatanisho wa kudumu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.