2016-02-12 09:45:00

Mwaka wa Neema ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuanza hija yake ya kichungaji nchini Mexico, Alhamisi, tarehe 11 Februari 2016 alitembelea Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu mjini Roma na kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wakati huu wa hija yake ya kitume nchini Mexico kuanzia tarehe 12 -18 Februari 2016. Baba Mtakatifu akapata pia nafasi ya kuwatembelea Wakleri wa Jimbo kuu la Roma waliokuwa wanafanya tafakari ya Kwaresima kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano na huko akawashirikisha chemchemi ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu!

Baba Mtakatifu Francisko anamshukuru Mungu kwa matukio mbali mbali yanayoendelea kujionesha wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Neema, Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Akiwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Baba Mtakatifu ameungama dhambi zake na pia kuwaungamisha baadhi ya Wakleri.

Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma amemhakikishia Baba Mtakatifu Francisko uwepo wa karibu wa Familia ya Mungu kwa njia ya sala wakati wote wa hija yake ya kitume nchini Mexico. Kanisa linaendelea kuadhimisha Jubilei ya huruma ya Mungu kwa shughuli mbali mbali za maisha ya kiroho zinazotekelezwa Parokiani, ili kila mtu aweze kuonja na hatimaye kuambata huruma ya Mungu katika maisha yake binafsi na kwa jirani wanaomzunguka.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu Francisko anawataka Mapadre kuhakikisha kwamba, wanaimwilisha huruma ya Mungu katika maisha na vipaumbele vya shughuli zao za kichungaji; kwa kuwafahamu watu wao, ili kuweza kuwaondolea dhambi, tayari kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Mapadre wawe ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa wale wote wanaokimbilia kwenye kiti cha maungamo, hapo wakutane na Padre mpole, mwema na mnyenyekevu, na kwa njia hii, waamini wajenge utamaduni wa kukimbilia mara kwa mara huruma ya Mungu katika maisha yao!

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, dhana ya Jubilei ya huruma ya Mungu ni wazo lililoanzishwa na Mwenyeheri Paulo VI; dhana hii ikamwilishwa kwa namna ya pekee na Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake; Mtakatifu Faustina Kolowaska na ujumbe wake, ukawa ni chachu ya kuenea kwa Ibada ya huruma ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia; Papa Mstaafu Benedikto XVI akaimarisha dhana ya huruma ya Mungu kwa njia ya Katekesi makini, ili kuliwezesha Kanisa kuwa kweli ni chombo cha huruma ya Mungu kwa waja wake.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawaalika Mapadre kuwa na moyo wa ukarimu na mapendo kwa wadhambi; tayari kuwaondolea dhambi na kuwaonjesha huruma ya Mungu. Mapadre wajitahidi kufahamu lugha wanayotumia waamini wao kuomba huruma na msamaha wa Mungu. Itakumbukwa kwamba, mkutano wa Wakleri wa Jimbo kuu la Roma ulipania kuwapatia fursa ya kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuwazamisha waamini wao katika mafuriko ya huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.