2016-02-12 09:04:00

Jikaneni, bebeni vyema Misalaba yenu, kisha mfuateni Kristo Yesu!


Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee katika kipindi hiki cha Kwaresima ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kujikana wenyewe; kubeba Misalaba yao na kisha kumfuasa Kristo; kama walivyofanya Watakatifu Padre Pio wa Pietrelcina na Leopoldo Mandic wakati wa uhai wao hapa duniani. Kwa njia hii, watakatifu hawa wakawa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu iliyotolewa kwa watu katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho.

Hivi ndivyo alivyosema, Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Uinjilishaji mpya Alhamisi tarehe 11 Februari 2016 wakati wa mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuaga Masalia ya Watakatifu Padre Pio na Leopoldo yaliyokuwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa takribani juma zima, ili kuwaalika waamini katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kukimbilia kwenye kiti cha maungamo, kwa kufanya toba, ili kuonja tena huruma na upendo wa Mungu! Wakati wa kurejesha masalia haya kwenye maeneo yake, Masalia ya Padre Pio wa Pietrelcina yamesimama kwa kitambo Benevento na Foggia kabla ya kuwasili na kuhifadhiwa huko San Giovanni Rotondo. Masalia ya Mtakatifu Leopoldo yamesimama kwa kitambo Loreto na Bologna na baadaye kuelekea Padua mahali ambako masalia haya yanahifadhiwa.

Askofu mkuu Fisichella anakaza kusema, Mtakatifu Leopoldo alitamani sana kuwa mmissionari, ili kujenga na kudumisha majadiliano na umoja; akataka kuwa mhubiri mahiri, lakini Mungu alikuwa na mpango tofauti kabisa katika maisha yake, akajikuta anazama katika ukimya kwenye kiti cha maungamo, hata wakati nyumba yao ya kitawa ilipolipuliwa, yeye akabaki mzima! Padre Pio kwa upande wake, alijitahidi kubeba Msalaba wa maisha na utume wake kila siku, huku akibeba Madonda matakatifu mwilini mwake, kielelezo cha mateso na kifo cha Kristo katika maisha yake. Padre Pio akawa kweli ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu iliyomwilishwa kwa waamini kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, ili waamini waweze kuonja ndani mwao maisha na msamaha wa dhambi.

Ibada hii imehudhuriwa na wajumbe wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya, Wafranciskani, Wakleri na waamini walei waliotumia Siku ya Alhamisi, tarehe 11 Februari 2016 kutoa heshima yao na kuomba huruma ya Mungu kwa njia ya watakatifu hawa, Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu! Kwaresima iwe ni fursa ya kusali, kufunga, kutubu, kuongoka na kumwilisha imani katika matendo ya huruma, kielelezo cha ushuhuda wa Ukristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.