2016-02-12 10:17:00

Hii ni hija inayohitaji nguvu za kiroho na kimwili!


Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima wakati akiondoka nchini Russia kuanza hija yake ya kichungaji Amerika ya Kusini aliwaambia waandishi wa habari kwamba, hii ni safari ndefu na nzito inayohitaji nguvu za kiroho na kimwili. Patriaki Kirill amewasili nchini Cuba, Alhamisi, tarehe 11 Februari 2016, huku akiwa ameambatana na ujumbe mzito wa viongozi wa kidini pamoja na waandishi wa habari. Katika hija yake ya kichungaji Amerika ya Kusini inayodumu takribani siku kumi na moja, anatembelea Paraguay na Brazil.

Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Umoja wa Wakristo amewasili nchini Cuba, Alhamisi tarehe 11 Februari 2016. Kabla ya kuondoka mjini Vatican, Kardinali Koch katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kwamba, mkutano kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima utasaidia kukuza na kukoleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene katika mwelekeo unaojikita kwanza kabisa uelewa binafsi na ule wa Makanisa yao, kuhusu mchakato wa kiekumene.

Kardinali Koch anasema, hizi ni cheche kwa viongozi wa Makanisa kuendelea kujenga utamaduni wa kukutana na kujadiliana na kwamba, huu ni mwanzo pia kwa viongozi wa Kanisa la Kiorthodox kuweza kukutana na kujadiliana, ili kupanua wigo wa majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa, tayari kushirikishana na kushikamana katika: Ukweli, upendo, sala na shuhuda zinazoendelea kutolewa na damu ya mashuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Hii ni changamoto pia kwa Kanisa la Kiorthodox ambalo kwa mara ya kwanza litafanya Sinodi mtambuka, huko Creta.

Hapa viongozi wa Kanisa watajadili kwa kina na mapana maisha na utume wa Kanisa la Kiorthodox. Patriaki Kirill anafahamu hali halisi ya Makanisa haya mawili pamoja na changamoto zake, lakini ameonesha ujasiri na ukomavu wa imani ili kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Hii ni hatua makini katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.