2016-02-12 07:38:00

Baba Mtakatifu Francisko nchini Mexico!


Mmissionari wa huruma na mjumbe wa amani ndiyo kauli mbiu inayoongoza hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Mexico kuanzia tarehe 12 – 18 Februari 2016. Baba Mtakatifu anapenda kukugusia kwa namna ya pekee: huruma, haki na amani; imani, matumaini na mapendo; Ibada kwa Bikira Maria wa Guadalupe pamoja na changamoto ya wahamiaji na magenge ya uhalifu. Hii ni hija inayojikita pia katika mchakato wa kiekumene,kwa Baba Mtakatifu Francisko kukutana na kuzungumza na Patriaki Kirill wa Mosco na Russia nzima.

Haya ndiyo mambo makuu ambayo yamezingatiwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV wakati huu wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu nchini Mexico. Baba Mtakatifu anapenda kukazia kwa namna ya pekee kwa wananchi wa Mexico kuwa wajenzi na mashuhuda wa haki, amani, mapendo na huruma; mambo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu, kwa kutambua kwamba, Familia ya Mungu nchini Mexico ina ibada ya pekee kwa Bikira Maria wa Guadalupe.

Baba Mtakatifu pia anapenda kugusia mambo yanayoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu; ustawi na maendeleo ya wengi. Rushwa na ufisadi; biashara haramu ya dawa za kulevya na madhara yake kwa vijana wa kizazi kipya; magenge ya kihalifu na uvunjaji wa sheria na kanuni msingi za maisha ya kijamii; umaskini pamoja na uhuru wa kuabudu. Mahusiano kati ya Serikali na Kanisa kwa miaka mingi hayakuwa mazuri, huu ni wakati muafaka wa kwa pande hizi mbili kuweza kushirikiana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu nchini Mexico. Ndiyo maana Baba Mtakatifu atazungumza na viongozi wa Serikali, wanasiasa na wanadiplomasia, ili kuonesha umuhimu wa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya mafao ya wengi.

Kardinali Parolin anafafanua kwamba, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu nchini Mexico inajikita katika Ibada kwa Bikira Maria wa Guadalupe, anayependa kujikabidhi kwake na kumtolea heshima yake, ili aweze kumsaidia katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu anataka kumkabidhi Bikira Maria wa Guadalupe: matatizo, changamoto na matumaini ya watu kutoka ndani na nje ya Mexico, ili aendelee kuwafariji na kuwao mbea huko mbinguni!

Baba Mtakatifu Francisko ni mmissionari wa huruma na mjumbe wa amani; mambo ambayo yanapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Familia ya Mungu nchini Mexico inaalikwa kwa namna ya pekee kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma ya Mungu, kama alivyo Baba yao wa mbinguni, tema inayoongoza maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kardinali Pietro Parolin anakaza kusema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Mexico inataka kuwaimarisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kupinga utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika rushwa na ufisadi; biashara haramu ya dawa za kulevya na magenge ya kihalifu yanayokwamisha mchakato wa maendeleo endelevu: kiroho na kimwili nchini Mexico.

Uhamiaji ni changamoto kubwa inayogusa na kutikisa misingi ya kifamilia na mafungamano ya kijamii. Kanisa limekua mstari wa mbele katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji, lakini linapaswa kujitoa zaidi kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha na matumaini. Familia ya Mungu inapaswa kuwa kweli mstari wa mbele ili kupambana na matatizo na changamoto zote hizi, ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Itakumbukwa kwamba, haya ni mambo ambayo Baba Mtakatifu pia aliyagusia wakati wa hija yake ya kitume kwenye Umoja wa Mataifa, Septemba 2015. Uhamiaji wa shuruti, biashara haramu ya silaha na dawa za kulevya ni mambo yanayoendelea kuandika kurasa chungu za maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu anayazungumza yote haya kutaka kuonesha ile hali ya Msamaria mwema anayeguswa na mahangaiko ya watu wake, ili kuwaonjesha huruma ya Baba wa milele.

Lakini, Mexico pia ina utajiri mkubwa wa utamaduni na mapokeo; rasilimali kubwa katika ustawi na maendeleo ya wengi nchini Mexico. Huu ni mwaliko wa kusimama kidete kupambana na mambo yote yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu, ili kusongesha mbele mchakato wa maendeleo endelevu! Kardinali Parolin anasema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Mexico ina mwelekeo pia wa kiekumene kwani Baba Mtakatifu Francisko tarehe 12 Februari 2016 akiwa njiani kuelekea Mexico anakutana na Patriaki Kirill wa Mosco na Russia nzima. Hili ni tukio la matumaini na ujasiri ili kujenga msingi wa majadiliano ya kiekumene baina ya Makanisa haya mawili pamoja na ustawi wa wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.