2016-02-11 07:56:00

Waislam na Wakristo shikamaneni kujenga na kudumisha amani Zanzibar


Askofu Augustino Shao wa Jimbo Katoliki Zanzibar anawahamasisha wanachama wa CUF na CCM kushikamana ili kujenga, na kudumisha haki, amani, ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Zanzibar, hasa wakati huu ambapo Zanzibar inajiandaa kwa ajili ya kurudia uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani Zanzibar, hapo tarehe 20 Machi 2016 baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu Zanzibar uliofanywa hapo tarehe 25 Oktoba 2015 kufutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar. Askofu Shao anawapongeza wananchi wa Zanzibar ambao tangu wakati huo wameonesha ukomavu wa kisiasa na utulivu.

Wanasiasa wanaendelea na mchakato wa majadiliano ya kisiasa, lakini waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo Visiwani Zanzibar wanapaswa kuendelea kushikamana katika upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa kwa ajili ya mafao ya wengi. Viongozi wa kidini wakati wote huu wameendelea kuwahimiza wananchi kuonesha ukomavu, utulivu na amani, ili hatimaye, suluhu ya kudumu iweze kupatikana Visiwani Zanzibar. Chama cha Wananchi CUF na Chama cha Mapinduzi, CCM vikiridhiana na kushirikiana, amani na utulivu vinaweza kupatikana na kudumishwa Visiwani Zanzibar.

Askofu Shao anakaza kusema tofauti na kinzani za kisiasa Visiwani Zanzibar zilisababisha kudumaa kwa maendeleo ya wengi, Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo imefanya kazi kwa muda wa takribani miaka mitano ilikwamua hali hiyo, amani na utulivu vikarejea tena Zanzibar. Kumbe, umoja na mshikamano wa kitaifa ni dhana inayowezekana anasema Askofu Shao wa Jimbo Katoliki Zanzibar. Waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo waendeleze mchakato wa majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi; kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, ustawi, mafao na maendeleo ya wote. Misimamo mikali ya kidini ni hatari kwa mafungamano ya kijamii na maendeleo ya watu kwani amani ni jina jipya la maendeleo endelevu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.