2016-02-11 15:31:00

Wagonjwa thubutuni kumkimbilia na kumtumainia Mungu!


Mama Kanisa tarehe 11 Februari 2016 anaadhimisha Siku ya 24 ya Wagonjwa Duniani ambayo kwa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu unaongozwa na kauli mbiu “ Kujiaminisha kwa Yesu mwenye huruma kama Bikira Maria. Lolote atakalowaambia fanyeni”. Wahudumu katika sekta ya afya wanakumbushwa kwamba, wanashirikishwa kwa namna ya pekee katika huduma ya Injili ya uhai, changamoto inayowahitaji kuwa kweli ni wajenzi wa utamaduni wa watu kukutana na kudumisha amani.

Huruma kwa wagonjwa ni kiini cha uchaji wa Mungu karama inayopaswa kudumishwa na wafanyakazi pamoja na wale wote wanaobahatika kuwahudumia wagonjwa, ili kumwilisha Imani na heri za Mlimani, ambazo kimsingi ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya KristoYesu! Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anapenda kuwakumbusha wagonjwa kwamba, Mwenyezi Mungu anatambua mateso na mahangaiko yao na anawajali. Wagonjwa wanapaswa kuthubutu kumkimbilia na kumtumainia Mungu.

Askofu mkuu Ruwaichi anawataka wagonjwa kwa namna ya pekee kutolea mateso yao ili yaunganishwe na mateso ya Kristo ili yafae kwa wokovu wa wagonjwa wenyewe na pamoja na wokovu wa wanadamu wengine, hasa wale ambao ni wahitaji Zaidi kadiri ya hali zao za kiroho. Kwa wale wanaowahudumia wagonjwa wawe ni wahudumu katika sektaya afya au ndugu na jamaa, watambue kwamba wao ni mkono wa Kristo katika kupeleka Huruma na Uponyaji kwa watu wake. Huu ni mwaliko kwa wahudumu katika sekta ya afya kutekeleza dhamana na wajibu huu nyeti kwa upendo, huruma, kwa kujituma na kwa uvumilivu mkuu pamoja na kutambua kwamba, kuna changamoto nyingi ambazo wanakabiliana nazo katika sekta ya afya. Askofu mkuu Ruwaichi anakaza kusema, wahudumu waone pia fursa walizokirimiwa na Mwenyezi Mungu, mapaji na maandalizi yote muhimu kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa, ili kutumia fursa hii kuwa ni chombo cha uponyaji wa Mungu kwa binadamu wenzao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.