2016-02-11 09:36:00

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya Kwanza ya Kwaresima Mwaka C


“Katika Waraka Uso wa huruma, maalum kwa ajili ya kuzindua Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu niliwaomba kwamba ‘Kwaresima ya Mwaka huu tuiishi kwa uzito zaidi kama muda mahsusi kwa kuadhimisha na kuonja huruma ya Mungu. Ni kurasa ngapi za Maandiko Matakatifu, zinaweza kutafakariwa katika majuma ya Kwaresima kwa lengo la kutusaidia kuugundua tena uso wa huruma wa Baba!” Kwa kifungu hiki cha maneno ndivyo Baba Mtakatifu Francisko anavyoanza ujumbe wake wa Kwaresima kwa mwaka 2016. Ni nukuu ambayo inatuelezea kwa kifupi kabisa maana na makusudi ya kipindi hiki katika mwaka wa Kanisa, yaani, ni majira yaliyowekwa mahasusi kabisa kwa kumrudia na kujipatanisha na Mungu kwa kufanya toba na wongofu wa ndani.

Katika Dominika hii ya kwanza ya Kwaresima, Mama Kanisa anatuwekea mbele yetu tafakari juu ya ushawishi wa shetani ambaye daima anatutafuta na kutushawishi kusudi tuweze kuacha kuutafuta uso wa huruma ya Mungu na kuingia katika dhambi. Lakini pia tunaoneshwa namna ya kumshinda huyu shetani na kumpatia Mungu utukufu. Hii ni tafakari nzuri tunayoanza nayo katika kipindi hiki cha toba kusudi tuweze kutambua kinagaubaga juu ya njia na mbinu za huyu muovu na kutafuta njia za kumwepa, yaani kutafuta namna ya kujishikamanisha zaidi na Mungu na kumkimbia shetani, na kwa kweli hili ndilo lengo la kipindi hiki cha Kwaresima. Mambo matatu yanatajwa katika Injili ambayo yanakusanya kwa ujumla vishawishi vyote vya mwovu shetani. Mambo hayo ni matamanio yetu ya kimwili, tamaa zetu katika mali za kidunia na tamaa zetu katika madaraka.

Mwili wetu huwa unapatwa na njaa za kila aina ambazo kwa bahati mbaya hutufumba macho na kushindwa kuyaona mapenzi ya Mungu. Tupo tayari kukurupusha ahadi zetu za ubatizo kusudi tuweze kujituliza na adha za kiulimwengu ambazo hupita baada ya kitambo. Hii ni changamoto inayowekwa mbele yetu ili kuona kwa jinsi tunavyomwacha Mungu na neno lake na kuchuchumilia faraja za kiulimwengu. Mali ni tamanio la kila mwanadamu. Watu wengi huangaika kwa ajili ya kutafuta kujilimbikizia mali. Utajiri huu wa kidunia hutugeuza kuwa waabudu wa nguvu za giza na kupoteza upendo wetu kwa Mungu na jirani zetu. Leo hii tunawaua ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi kwa ajili ya kupata mali; leo hii tunawanyonya watu haki zao za msingi kusudi tu tuzidi kujilimbikizia utajiri. Badala ya kuwa na furaha au uhuru tunafanywa kwa watumwa wa mali za kidunia. Madaraka na vyeo vya kidunia hutufanya tujione kuwa ni miungu katika jamii. Mwanadamu wa leo anachuchumilia nafasi hizi za kimadaraka ili kupata jina kubwa na umaarufu kati ya watu.

Changamoto zote hizi tatu hutuweka mbali na Mungu. Kristo leo hii anakuja kwetu kama mfano wa namna ya kuzishinda na kumpatia Mungu utukufu. Mtume Paulo anatuambia katika somo la pili kwamba “ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka”. Bwana wetu Yesu Kristo anajidhihirisha kwetu kwamba Yeye ndiye njia tunayopaswa kuifuata katika kupingana na shetani na kumtii Mungu. Alikuwa tayari kuitii sauti hiyo ya Mungu hadi akapokea kifo cha Msalaba. Kwa njia yake nasi tuliopokea hadhi ya kuitwa waana warithi wa Mungu tunaalikwa kujiweka katika hali ya kugutuka na kuiepa mitego ya shetani katika juhudi zetu zetu za kila siku za kumtukuza mwenyezi Mungu kwa maisha yetu.

Tunalojifunza kwa Kristo ni fadhila ya unyenyekevu. Kinyume cha fadhila hii ni kiburi na majivuno. Kristo anatuonesha kwamba ni kwa njia ya kuwa tayari kujishusha na kujitambua nafasi yako mbele ya Mwenyezi Mungu na kuanza kuhusiana  naye kama Baba yetu mwema. Yeye anatupenda daima na ulimwengu wote aliouumba vizuri ametukabidhi ili kuuratibu vema. Tunapaswa kumpatia Yeye heshima inayomstahili kwa sala zetu za shukrani na kwa sadaka zetu na tutalifanikisha ili pale tu tutakapokuwa tayari kuyafanya yale yaliyo mapenzi yake. Leo hii tunajiondoa katika hadhi hii nzuri ya kuwa watoto wa Mungu. Tamaa zetu za kidunia zinatufunika kiasi cha kushindwa kuuona wema wa Mungu. Tunapata wapi wasiwasi wa kuwa na ulimwengu huu na mali zake wakati mwenyezi Mungu mwenyewe amekwisha tupatia tuutunze? Hapa kweli ndipo tunapopaswa kuistukia kazi ya adui mwovu shetani.

Mwanadamu anapomkaidi Mungu anaingia katika hali ya utumwa. Sehemu ya kwanza ya somo la kwanza inalionesha ili kwa njia ya ishara ya Taifa la Israeli ambao walikuwa taifa teule la Mungu lakini pale waliamua kwenda kukaa ugenini Misri waliishia kuwa watumwa karibu kupotea. Lakini sehemu ya pili ya somo hilo inatufunulia uso wa Baba mwenye huruma ambaye anashuka na kuwarudishia tena utu wao wale aliowachagua, wale aliowapenda. Hapa tunapata kwa ufupi mwaliko wa toba na wongofu wa ndani tayari kuambata huruma ya Mungu. Mungu wetu mwenye huruma alitupatia nchi ya ahadi iliyo na kila aina ya wema wake, lakini bado tunataka kukimbilia ugenini ambako tunaishia katika utumwa: tunakuwa watumwa wa pesa na madaraka, watumwa wa vyeo na umaarufu, watumwa wa tafrija na anasa na mengineyo mengi ya kidunia yanayotufunga. Fungua macho yako, ikimbilie huruma ya Mungu.

Antifona ya mwanzo ya Dominika hii inatupatia maneno ya matumani: “Ataniita nami nitamwitikia; nitamwokoa na kumtukuza; kwa siku nyingi nitamshibisha.” Ni mwaliko huo wa mwenyezi Mungu, Baba yetu mwenye uso wa huruma ambaye yupo tayari mlangoni kutupokea, kutubusubusu, kutusafisha na kutuvisha vazi lililo bora zaidi. Mtume Paulo alitualika siku ya Jumatano ya majivu: “Wakati uliokubalika nalikusikia, siku ya wokovu nilikusaidia; tazama, wakati uliokubalika ndiyo sasa; tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa”. Ndiyo wakati huu wa Kwaresima na kwa namna ya pekee katika mwaka huu wa huruma ya Mungu. Tuikimbilie basi huruma hii ya Mungu kwa toba, tumrudie Mungu wetu kwani daima yupo tayari kutupokea.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.