2016-02-09 10:39:00

Zingatieni miiko na maadili ya kazi!


Ifuatayo ni hotuba ya Mhe. Ummy Mwalimu (MB) Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto nchini Tanzania katika uzinduzi wa Baraza la optometria, Baraza la wataalamu wa radiolojia, na Bodi ya maabara binafsi tarehe 8 Februari, 2016. Ndugu Wenyeviti/Wajumbe wa Mabaraza na Bodi, Napenda kutoa shukrani za dhati kupata fursa hii ya kufanya uzinduzi wa Baraza la Wataalamu wa Kurekebisha Upeo wa Macho Kuona (Optometria), Baraza la Wataalamu wa Radiolojia na Bodi ya Maabara Binafsi. Ingawa hafla kama hii huchukua muda mfupi, kwa upande wangu naipa umuhimu mkubwa kwa vile ni muda adimu ninaoweza kuonana nanyi kujadiliana nanyi na pia kutoa maelekezo ya nini kifanyike katika utumishi wenu ndani ya Mabaraza na Bodi. Aidha, hafla kama hizi zinatoa nafasi ya kutathmini huduma mbalimbali zinazotolewa na kuwafahamisha wananchi kuhusu huduma hizo kwa lengo la kufanikisha utoaji wa huduma bora za Afya nchini.

 Ndugu Wenyeviti/Wajumbe wa Mabaraza na Bodi, Nikiwa Waziri mwenye dhamana ya kusimamia Mabaraza na Bodi zote za Kitaalamu, napenda kuchukua nafasi hii ya kipekee kuwakaribisha na kuwapongeza; Wenyeviti pamoja na Wajumbe wote mlioteuliwa kutumikia Mabaraza na Bodi kwa kipindi cha miaka mitatu yaani mwaka 2015-2018. Kwa namna ya pekee, nitumie fursa hii kuwashukuru ninyi wote kwa kukubali uteuzi huu. Hongereni sana. Aidha, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa wote walioshiriki katika maandalizi ya uzinduzi huu.

Ndugu Wenyeviti/Wajumbe wa Mabaraza na Bodi, Mabaraza na Bodi ya Kitaalamu ni vyombo vya Kisheria vyenye mamlaka ya kusimamia Wataalamu, vituo vinavyotoa huduma za kitaalamu, Vifaa, vitendanishi na ukusanyaji wa mapato. Majukumu ya kusimamia utoaji huduma bora za afya kwa jamii yana umuhimu mkubwa sana na yanahitaji mwendo wa kasi. Na hili ni muhimu sana hasa katika awamu hii inayozingatia na kutekeleza dhana ya Hapa Kazi tu.  Mabaraza ya Optometria, Radiolojia na Bodi ya Maabara Binafsi na Bodi yana wajibu wa kuhakikisha Wataalamu wanawajibika kutenda majukumu yao kwa kufuata maadili ya taaluma husika. Aidha, Mabaraza na Bodi hizi ndio vyombo pekee vinavyohakikisha maadili ya taaluma yanafuatwa na kuhakikisha kuwa wale wote wasioendana na maadili hayo wanachukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa Sheria.


Ndugu Wenyeviti/Wajumbe wa Mabaraza na Bodi, Nimefurahi kusikia kwamba Mabaraza na Bodi za Kitaalamu mmeweza kutimiza majukumu yenu kwa kufanya vikao vya kisheria ingawa vingine havikufanyika kwa wakati muafaka. Naendelea kusisitiza kwamba vikao hivi ni muhimu sana ukizingatia ndio vinavyothibitisha usajili wa wataalamu, vituo na vitendanishi, kucheleweshwa kwa vikao hivi kutazorotesha huduma hii na kusababisha usumbufu na kuleta malalamiko yasiyo ya lazima. Natambua katika vikao hivyo idadi ya waliosajiliwa, kuandikishwa, na kuorodheshwa inaendelea kuongezeka katika kila fani. Aidha nasisitiza kuwa mfanye vikao vyenye kuleta matokeo ya kiutekelezaji (deliverables) kwa kufuata taratibu zilizowekwa.

Ndugu Wenyeviti/Wajumbe wa Mabaraza na Bodi, Suala lingine ni la miiko na maadili (code of ethics and professional conduct) kwa Wataalamu wa afya linaloendana na ‘stadi za kazi’; Mabaraza na Bodi inabidi yahakikishe maadili ya kazi kwa Wataalamu yanasimamiwa kikamilifu. Na wale wote wanaokiuka maadili ya kazi ni wajibu wa mabaraza kuchukua hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo. Nikiwa na dhamana ya kusimamia Sekta ya Afya sitakubali kusikia mtaalamu au wataalamu wanakiuka maadili kwa kuendekeza maslahi binafsi, kujihusisha na vitendo vya rushwa, kutokuwajibika ipasavyo na mambo yanayofanana na hayo. Na hapa napenda kutoa rai kwa Wataalaamu wote wa afya nchini kuhakikisha kwamba maadili ya kazi yanafuatwa kwa ukamilifu bila ya kuwa na kigugumizi. Ninatambua kuwa vitabu vya Miiko na Maadili kwa Wataalamu wa Mabaraza yote vimetolewa. Naagiza vitabu hivyo visambazwe kwa Wataalamu wote ili wavisome na kuvielewa.


Ndugu Wenyeviti/Wajumbe wa Mabaraza na Bodi, Utaalamu bila kuwa na ujuzi (professional skills) ni butu. Napenda kusisitiza kuwa, elimu ya kujiendeleza (Continuous Professional Development) kwa wataalam wetu. Ninyi mkiwa ndio watunga sera na waonyesha dira inabidi Mabaraza yenu yawe na juhudi za ziada kuhakikisha Wataalamu wanahamasishwa kujiendeleza katika maeneo yao ya kazi; kupitia mitandao na majarida mbalimbali ya kitaaluma. Lengo hasa likiwa ni kuwa na ufanisi katika utoaji wa huduma bora za afya kwa maendeleo ya jamii. Kutokana na umuhimu wake suala hili lipewe kipaumbele, na msisitizo huu ni kwa Mabaraza na Bodi zote za kitaalamu.

Ndugu Wenyeviti/Wajumbe wa Mabaraza na Bodi,  Ninaagiza pia usajili wa Vifaa na vitendanishi uendelee kupewa kipaumbele ili kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa ziwe na ubora unaokubalika kitaifa na kimataifa ikiwa ni pamoja na kutoa majibu sahihi ya vipimo. Ukaguzi wa mara kwa mara ufanyike ili kuratibu shughuli za vituo vinavyotoa huduma hizo. Nimefurahishwa na Mchakato wa kuundwa kwa kamati elekezi ya Mabaraza na Bodi zote (Steering Committee) chini ya Mganga Mkuu wa Serikali, kwani kwa kufanya hivyo mtarahisisha utendaji kazi na kuleta ufanisi. Naagiza rasimu ifanyiwe kazi haraka ili kupata nyaraka halisi na kuwezesha Kamati elekezi kutimiza majukumu yake.

Ndugu Wenyeviti/Wajumbe wa Mabaraza na Bodi, Nimepokea changamoto zenu mlizonieleza zenye masuala mtambuka (cross cutting issues) katika utoaji huduma ya afya. Ni jukumu la Mabaraza na Bodi kukaa pamoja na kupata ufumbuzi katika masuala haya ili kuepuka mgongano wa kimaslahi (conflict of interest) wa wataalamu mnaowasimamia. Vilevile masuala ya uhaba wa fedha yaendelee kujadiliwa kupitia kwenye vikao vya Mabaraza na Bodi, Kamati elekezi (steering committee) na vikao vya menejimenti vya Wizara. Kwa yale ambayo yanahitaji utatuzi wa muda mrefu kama uhaba wa Ofisi, Usafiri na uhaba wa vyuo nitayachukua, na ninaahidi kuyafanyia kazi.

Ndugu Wenyeviti/Wajumbe wa Mabaraza na Bodi, Siku hizi kumekuwa na matumizi makubwa ya vyeti vya kughushi, vikiwemo vya vituo vya kutolea huduma na Wataalamu. Watu wasio na taaluma wanatoa huduma za kitaalam. Suala hili halikubaliki na halivumiliki. Mabaraza na Bodi yana mamlaka (mandate) ya kumchukulia hatua za kinidhamu pale inapobainika mtu anatoa huduma kinyume cha sheria. Aidha, elimu ya kitaaluma (advocacy) itolewe mara kwa mara kwa wananchi kupitia vyombo vya habari kama ‘television’, radio, magazeti n.k. ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na ufahamu kuhusu huduma bora za afya zitolewazo na Wataalamu husika. Wananchi wakielimishwa watawaepuka watoa huduma batili wasiokuwa na utaalamu na ujuzi. Mabaraza na Bodi ni vyombo pekee vinavyohakikisha mambo haya hayatokei; na ninaamini kwamba Mabaraza na Bodi yanauwezo mkubwa wa kufuatilia masuala haya kwa mujibu wa Sheria. Naomba msisite kushirikiana nami pale mnapo hitaji msaada wangu.

Ndugu Wenyeviti/Wajumbe wa Mabaraza na Bodi, Si nia yangu leo kutoa hotuba ndefu, huu ni ufafanuzi tu wa kile kinachotakiwa kufanyika kulingana na dira na kasi ya serikali ya awamu ya tano, katika kuboresha afya, nguvu kazi na maendeleo ya wananchi. Serikali haitavumilia au kusita kuvunja Baraza au Bodi yoyote kwa kutokutekeleza majukumu yake kama yalivyofafanuliwa katika sheria husika.

 Ndugu Wenyeviti/Wajumbe wa Mabaraza na Bodi,  Kufuatia uteuzi wa Wajumbe wa Mabaraza na Bodi, natoa maagizo ya utekelezaji kama ifuatavyo:- Mabaraza na Bodi yafuatilie utekelezaji wa Sheria za Mabaraza husika kwa kuzisoma kwa makini, kuzielewa, kuzisimamia na kuzitekeleza. Uteuzi wa Wasimamizi wa Mikoa na Wilaya kwa kipindi cha 2015 -2018 ufanyike kama Sheria zinavyoelekeza. Kila Baraza na Bodi iandae mpango mkakati (strategic plan) wa kiutekelezaji wa Sheria husika. Mabaraza na Bodi yaainishe vyanzo vya mapato kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli zao, Mabaraza na Bodi yawe na mfumo wa Kielekroniki katika kutekeleza majukumu yake.

Ndugu Wenyeviti/Wajumbe wa Mabaraza na Bodi, Mwisho, moja ya kazi za Mabaraza na Bodi ni kuhakikisha Wataalamu wote, vifaa na vitendanishi vinasajiliwa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na taratibu zilizowekwa. Kwa hiyo hakikisheni wataalamu wote, vifaa na vitendanishi vinavyohusika katika utoaji wa huduma za afya vinasajiliwa kwa mujibu wa Sheria husika. Na wale ambao watakaidi hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao. Ukusanyaji wa mapato ni eneo lingine nyeti, hakikisheni maduhuli yanakusanywa ipasavyo na kwa muda muafaka.

Ndugu Wenyeviti/Wajumbe wa Mabaraza na Bodi, Kwenye Mabaraza na Bodi za kitaaluma kuna wataalamu mbalimbali, wapo Madaktari, Wananasheria, Wataalamu wa fani husika, Wadau mbalimbali na Wakurugenzi kutoka hapa Wizarani. Watumieni hawa vizuri na kuhakikisha sera na miongozo ya kiutendaji wa kazi zinafuatwa kadri inavyoelekezwa na Wizara yangu mkiongozwa na Sheria, Kanuni za Mabaraza na Bodi. Baada ya kusema hayo, ninayofuraha kutamka kuwa Mabaraza ya Wataalamu wa Optometria, Radiolojia na Bodi ya Maabara Binafsi za Afya sasa yamezinduliwa rasmi.








All the contents on this site are copyrighted ©.