2016-02-09 09:31:00

Wamissionari wa huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano ya Majivu, tarehe 10 Februari 2016 siku ya kufunga na kusali, tayari kuanza kipindi cha Kwaresima ya Mwaka wa Huruma ya Mungu,  majira ya saa 11:00 za Jioni kwa saa za Ulaya ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na katika Ibada hii, atawatuma wamissionari 1, 071 wa huruma ya Mungu kwenda sehemu mbali mbali za dunia, ili kuwaondolewa watu dhambi ambazo kimsingi zinaondolewa tu na Vatican.

Hivi ni kati ya vielelezo makini vya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Uso wa huruma anafafanua kwamba, Wamissionari wa huruma ya Mungu watakuwa ni ishara ya hamasa ya kimama kwa taifa la Mungu, wakiwezeshwa kuingia kwa undani katika utajiri wa Fumbo msingi la imani. Hawa ni Mapadre ambao watapewa mamlaka ya kuondolea dhambi ambazo kwa kawaida zinazondolewa na Kiti cha Kitume pekee. Mapadre hawa watakuwa hasa ishara hai ya namna Baba mwenye huruma anavyowapokea wale wanaotafuta msamaha.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hawa ni wamissionari wa huruma ya Mungu kwa sababu watakuwa ni wawezeshaji kwa wote, huku wakiwa mwamesheheni ubinadamu, chimbuko la wokovu, uliojaa wajibu katika kushinda vikwazo, tayari kutweka hadi kilindini ili kuanza maisha mapya ya Ubatizo. Wamissionari hawa katika utume wao wanaongozwa na kauli mbiu “Mungu amewafunga wote pamoja katika kuasi ili awarehemu wote” (Rej. Rom. 11: 32).

Baba Mtakatifu anawahimiza Maaskofu Mahalia kuwaalika na kuwapokea wamissionari hawa, ili waweze kuhamasisha watu kupokea huruma ya Mungu pamoja na kuwatangazia furaha ya Injili ya msamaha. Maaskofu wenyewe pia wanaombwa kuadhimisha Sakramenti ya Upatanisho kwa watu wao, ili waamini wengi zaidi waweze kuguswa na hatimaye, kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Kipindi cha Kwaresima, iwe fursa kwa waamini wengi zaidi kukimbilia kwenye kiti cha huruma ya Mungu, ili kupata msamaha, neema na baraka ya kumshuhudia Kristo katika maisha yao! Sheria za Kanisa zinataja dhambi zifuatazo kuwa zinaweza kuondolewa tu kwa idhini ya Kiti cha Kitume: Kufuru kwa Ekaristi Takatifu; Madhara ya kimwili kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro; Kumweka Askofu wakfu pasi na ridhaa ya Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kumwondolea mwamini dhambi ambaye wote wawili wanahusika, yaani dhambi ya kuzini. Wale wanaotoa siri za maungamo. Pamoja na dhambi hizi, lakini Baba Mtakatifu Francisko anataka wale wote wanaojisikia kuwa mbali na huruma ya Mungu kutumia fursa hii kutubu, kuongoka na kuambata huruma hii katika maisha yao. Huu ndio wakati uliokubalika wa kutubu na kuongoka; ni fursa ya kumwachia Mungu nafasi ili aguse nyoyo za watu; ni nafasi ya kusikiliza kilio cha wadhambi, ili kuwarejeshea tena utu na heshima yao kama binadamu. Ikumbukwe kwamba, Kanisa ni chemchemi ya huruma ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.