2016-02-09 07:33:00

Papa nchini Mexico: Mmissionari wa huruma na mjumbe wa amani


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa familia ya Mungu nchini Mexico anasema kwamba, anakwenda kwao kama mmissionari wa huruma ya Mungu na mjumbe wa amani na kwamba, kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 18 Februari 2016 atakuwa pamoja nao na kwamba, tangu wakati huu anawakumbuka katika sala na sadaka yake. Baba Mtakatifu anasema, anawabeba ndani ya moyo wake na kwamba, anakwenda kutembelea nchi hii ambayo imebarikiwa na kupendwa sana na Mwenyezi Mungu pamoja na Bikira Maria.

Baba Mtakatifu anasema nia yake kuu ni kuwatembelea wananchi wa Mexico kama mmissionari wa huruma ya Mungu na mjumbe wa amani; anataka kukutana ili kwa pamoja waweze kuungama imani yao kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kushirikishana kweli za maisha; kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda sana watu wake kwa upendo usiokuwa na mipaka licha ya mapungufu yao ya kibinadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, anapenda kuwa karibu nao kadiri inavyowezekana, lakini zaidi na wale wanaoteseka, ili kuwakumbatia na kuwaambia kwamba, kweli Yesu anawapenda na daima yuko pamoja nao!

Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru kwa maandalizi makini wanayoendelea kufanya hadi sasa, zaidi kwa njia ya sala. Sala inapanua mioyo na kuweza kuiandaa ili kupokea zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Sala inaangaza macho ya watu ili kuweza kuangalia kama Mungu anavyoangalia; kupenda kama Mungu anavyopenda. Baba Mtakatifu anawashukuru wananchi wa Mexico kwa kusali na kumwombea katika maisha na utume wake.

Baba Mtakatifu anasema, hamu yake kuu ni kutaka kutembelea Madhabahu ya Bikira Maria wa Guadalupe kama mtoto anayetaka kumshirikisha Mama yake mpendwa yale yote yanayosheheni katika sakafu ya moyo wake, ili kuonja wema na upendo wake wa kimama; anataka kumwangalia machoni na kumwomba ili aendelee kuwangalia watoto wake kwa macho yenye huruma, kwani Bikira Maria, ni mama yao wa mbinguni. Baba Mtakatifu anapenda kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wakati huu wa hija yake ya kumi na mbili ya kimataifa nchini Mexico.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.