2016-02-08 15:43:00

Watawa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu!


Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ni matukio ambayo yanawakumbusha watawa kwamba, wao wameitwa, wakachaguliwa na kutumwa na Mama Kanisa kwenda sehemu mbali mbali za dunia, ili kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa njia ya karama za mashirika ya kitawa na kazi za kitume, zinazomwilishwa katika maisha na huduma mbali mbali kwa ajili ya Familia ya Mungu.

Mwenyezi Mungu anatambua nguvu na udhaifu wa watawa katika maisha na utume wao, lakini hawa bado wanaendelea kuwa ni vyombo vya huruma na mapendo kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro, mwamba wa imani aliyejaribiwa na wakati mwingine akajikuta akimkana Kristo kiasi cha mtu mzima kutokwa na chozi mbele ya umati wa vijakazi! Hii ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Patriaki Fouad Twal wa Yerusalem wakati wa kufunga maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mataifa, kwenye Mlima wa Mizeituni.

Maadhimisho haya yaliwashirikisha watawa wa mashirika mbali mbali wanaotoa huduma yao Nchi Takatifu, ambao walibahatika pia kupita kwenye Lango la Huruma ya Mungu, mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata Huruma ya Mungu katika maisha na utume wao. Watawa kwa njia hii wameadhimisha pia Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, mwendelezo wa tafakari makini walizofanya watawa katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, tayari kupyaisha maisha yao kwa kuendelea kusoma alama za nyakati.

Pariaki Twal anasema, Kristo alilaani sana dhambi, lakini akamkumbatia mdhambi na kumpatia nafasi ya kutubu na kumwongokea Mungu ili kuonja huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kama alivyofanya kwa mwana mpotevu anayesimliwa Mwinjili Luka na katika sehemu ya Injili ya Baba mwenye huruma. Wataw wawe mstari wa mbele kuwapelekea na kuwashirikisha watu huruma ya Mungu kwani wao kimsingi ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu.

Mama Kanisa anasema Patriaki Twal anatumwa kutangaza, kushuhudia na kumwilisha Injili ya huruma ya Mungu katika maisha ya watu, kwa kuwajengea matumaini kwamba, hata katika shida na mahangaiko yao ya ndani, bado kwa huruma ya Mungu wanaweza kuanza upya na kusonga mbele katika maisha na utume wao. Yesu Kristo anaendelea kutembea na watu wake, ili kuwainua na kuwaimarisha pale wanapoanguka kutokana na udhaifu wao wa kibinadamu, tayari kusonga mbele kwa kuambata huruma ya Mungu!

Katika mahubiri yake, Padre Pierbattista Pizzaballa, Mtunzaji mkuu wa Maeneo Matakatifu katika Nchi Takatifu amekazia kwa namna ya pekee, uhusiano uliopo kati ya maisha ya kitawa na kazi za kitume pamoja huruma ya Mungu. Mwaka wa Watawa Duniani kimekuwa kweli ni kipindi cha neema inayoendelezwa katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Huruma ya Mungu ni kiini cha maisha na utume wa wafuasi wa Kristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.