2016-02-08 15:31:00

Simameni kidete kutetea na kushuhudia Injili ya uhai!


Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, tarehe 7 Februari 2016 limeadhimisha Siku ya 38 ya Maisha Kitaifa ambayo imeongozwa na kauli mbiu “Huruma inachipusha maisha”. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, jumapili, ameungana na Maaskofu Katoliki Italia na wadau mbali mbali ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya maisha tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.

Jamii inapaswa kusaidiwa kuondokana na utamaduni wa kifo unaoendelea kushika kasi ya ajabu, kwa kufanya mageuzi ya ndani yanayoshuhudiwa kwa namna ya pekee na matendo ya huruma. Baba Mtakatifu amewapongeza wanafunzi na majaalim wa taasisi na vyuo vikuu vya Roma wanaoendelea kushuhudia Injili ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika ujumbe wake kwa maadhimisho haya linawakumbusha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, binadamu ni ndoto ya Mungu na anawapenda na kweli anataka wafanye mageuzi katika maisha yao kwa kukumbatia na kuambata huruma ya Mungu ambayo imewaletea maisha mapya. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni fursa ya kuondoa chachu ya zamani na unafiki kama Mafarisayo tayari kuambata upya wa maisha kwa kuwa na moyo thabiti unaobadili maisha kuwa kweli ni zawadi. Kwa njia hii ndoto ya Mungu inaweza kutendeka.

Maaskofu wanakaza kusema, ukuaji wa binadamu ni matunda ya neema ya Mungu inayojikita katika upendo thabiti kati ya bwana na bibi. Familia kadiri ya mpango wa Mungu kwa binadamu inaendeleza maisha. Kila mtoto anayezaliwa duniani ni sura ya Mungu anayependa na kuthamini maisha, zawadi kwa wazazi wake na jamii katika ujumla wake. Kila mtoto anayetolewa mimba anaongeza umaskini katika jamii. Kuna mamillioni ya watoto ambayo yametolewa mimba aliwahi kusema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kwa kisingizio cha kupambana na umaskini, lakini kimsingi ni kukumbatia utamaduni wa kifo.

Italia inaendelea kukabiliana na idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa hii inatokana na sera mbaya kuhusiana na familia. Serikali imeendelea kuwekeza kwa makundi madogo ya watu na kusahau familia zinazokabiliana na hali ngumu ya maisha pamoja na ukosefu wa fursa za ajira. Jamii inaweza kukua kwa nguvu na katika ubora ikiwa kama inajikita katika tunu msingi za maisha ya kifamilia. Familia ni kama shule inayowawezesha watu kupata mwelekeo mpana zaidi wa maisha na kuiwezesha jamii kukua na kukomaa katika utu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linawaalika waamini kuwa ni wajenzi wa madaraja ya watu kukutana ili kurithisha nguvu ya Injili inayoponya na kuganga woga usiokuwa na mvuto wala mashiko wa kujisadaka tayari kujenga utamaduni wa kukutana. Ni wajibu wa Kanisa kuendeleza mchakato wa majadiliano unaojikita katika Injili ya huruma ya Mungu, tayari kutoa majibu muafaka kwa familia zinazokabiliana na shida pamoja na changamoto za maisha, tayari kuwahamasisha watu kukumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Ni ndoto ya Mungu kujenga familia moja ya binadamu, pale tu binadamu atakapojifunza kutetea Injili ya uhai kwa kudumisha upendo na umoja wa kidugu katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Wale wote wenye dhamana ya kuhudumia Injili ya uhai watambue kwamba, wanashiriki katika kukamilisha ndoto ya Mungu dhidi ya utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba; ukosefu wa usalama kazini, vitendo vya kigaidi, vita, utapiamlo na kifo laini au Eutanasia.

Maaskofu wanasema, kupenda na kuthamini maisha ni kujitaabisha kwa ajili ya huduma kwa jirani, kwa kuonesha mapenzi mema; kwa kuheshimu na kudumisha utu wa mwanadamu na kwamba, huruma ya Mungu ni jina jipya la amani duniani. Huruma inachipusha maisha hata ya wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta hifadhi Barani Ulaya; watoto wanaopelekwa mstari wa mbele; wazee wanaotengwa na kunyanyaswa; watoto wanaotolewa wangali mimba. Kuambata huruma ya Mungu maana yake ni kongoka kutoka katika undani wa maisha kwa kuambata matendo ya huruma yanayotangaza utajiri wa binadamu, yanayokaa katika imani ya mafungamano ya kijamii, yanayoelimisha maisha bora ya Kiinjili na kuleta mabadiliko katika dunia kadiri ya ndoto ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.