2016-02-08 14:59:00

Huruma ya Mungu ni msingi wa haki zote!


Watu wanaohukumiwa na Mahakama za Vatican ni watu wenye mafumbo makubwa katika maisha; ni watu wenye mapungufu yao ya kibinadamu, lakini pia ni watu wenye utu na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Pietro Parolin, katibu mkuu wa Vatican, Jumamosi tarehe 6 Februari 2016 wakati wa kuzindua Mwaka wa 81 wa shughuli za Mahakama mjini Vatican.

Katika mahubiri yake, Kardinali Parolin amegusia mafanikio, matatizo na changamoto ambazo zimejitokeza mjini Vatican kwa kuwataka Majaji na  mawakili kuhakikisha kwamba, wanajikita katika tunu msingi zinazofumbatwa katika taaluma yao, ili kuhakikisha kwamba, haki inatendeka badala ya kufanya kazi kwa mazoea. Ili kutekeleza dhamana hii nyeti ya kuamua kilicho kweli na haki kunahitaji kuzama katika sheria inayotekelezwa kwa busara na uwiano bora. Jaji, kimsingi anapaswa kukumbatia unyenyekevu na ukweli wa mambo.

Kardinali Parolin anakaza kusema, kazi ya kuhukumu watu wengine ni nyeti sana na wala si tu suala ya kutekeleza mamlaka dhidi ya watu wengine, ingawa hili ndilo linaloonekana kwa wengi. Lakini kuna umuhimu mkubwa wakuhakikisha kwamba haki inatendeka kwa kujikita katika huduma inayotoa wakati mwingine maamuzi machungu, lakini kwa ajili ya mafao ya wengi. Majaji wawe na unyenyekevu na mpango mzuri wa kazi zao, ili kutenda katika misingi ya ukweli na uwazi; utulivu na huruma badala ya kumezwa na mambo mengi yanayoweza kuwavuruga na hivyo kushindwa kufanya kazi yao barabara.

Kardinali Pietro Parolin amehitimisha mahubiri yake kwa kukumbusha kwamba, katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Majaji wanapaswa kujifunza kuwa na huruma kwani Huruma ya Mungu, kimsingi ndiyo haki yake; mambo yanayoshikamana na kukamilishana. Ibada hii ya Misa takatifu imehudhuriwa na viongozi wakuu wa Kanisa, Majaji na wafanyakazi wa Mahakama za Kanisa mjini Vatican, wakuuu wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wageni waalikwa kutoka kwenye Mahakama za Italia. Baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, kumezinduliwa maadhimisho ya shughuli za Mahakama mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.