2016-02-08 15:13:00

Biashara ya binadamu ni uhalifu dhidi ya ubinadamu!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 7 Februari 2016 amekumbusha kwamba, Jumatatu tarehe 8 Februari 2016 ni Siku ya Sala na Tafakari dhidi ya biashara haramu ya binadamu, iliyoanzishwa mwaka mmoja uliopita, sanjari na kumbu kumbu ya Mtakatifu Josephine Bakhita kutoka Sudan, aliyeokolewa utumwani, akabahatika kubatizwa na hatimaye akawa ni mtawa wa Shirika la Wakanosa.

Katika maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo, Baba Mtakatifu Yohane Paulo II akamtangaza kuwa Mtakatifu. Hii ni fursa ya kusimama kidete ili kuwasaidia watu wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu katika ulimwengu mamboleo. Hawa ni watu wanaodhulumiwa na kunyanyaswa utu, heshima na uhuru wao kama binadamu.

Baba Mtakatifu anawakumbuka watu wote wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu, kumbe, kuna haja ya kusimama kidete ili kukomesha kabisa biashara hii haramu inayoendelea kuchefua utu wa binadamu! Takwimu zinaonesha kwamba, hadi wakati huu kuna zaidi ya watu millioni ishirini na moja waliogeuzwa kuwa watumwa wa ngono, biashara haramu ya viungo vya binadamu na kazi za suluba sehemu mbali mbali za dunia. Biashara hii haramu inawaingizia mafisadi kiasi cha dolla za kimarekani billioni thelathini na mbili kwa mwaka.

Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Ulimwenguni linaadhimisha siku hii kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kuongozwa na kauli mbiu “ Jubilei ya huruma ya Mungu kwa ajili ya uhuru wa watumwa mamboleo”. Baba Mtakatifu Francisko kwa nyakati tofauti amekaza kusema, biashara haramu ya binadamu ni uhalifu dhidi ya ubinadamu. Hii ni kashfa kubwa kwa ulimwengu mamboleo unaojidai kustaharabika. Ni nafasi ya kuchunguza dhamiri binafsi mbele ya Mwenyezi Mungu, tayari kutubu na kuambata huruma ya Mungu!

Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na kazi za kitume wanasema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni muda muafaka wa kupokea na kutumia huruma ili kuwasaidia wahanga wa utumwa mamboleo ili kuvunjilia mbali minyororo inayoendelea kuwabana katika utumwa, kiasi cha kuwanyima uhuru na kuendelea kudhalilisha utu wao kama binadamu. Lengo la siku hii ni kuwafahamisha watu madhara ya biashara haramu ya binadamu ili kuamsha dhamiri nyofu, tayari kusimama kulinda, kutetea na kuwasaidia wahanga wa biashara hii inayoendelea kushamiri kama uyoga!

Baba Mtakatifu Francisko ambaye ameendelea kulivalia njuga suala hili na biashara haramu ya binadamu aliwahi kusema kwamba, kuna haja ya kuhakikisha kuwa watu hawa wanapewa haki zao msingi, uhuru na utu wao kama binadamu unaheshimiwa na kuthaminiwa; kwa kuwaonesha ukarimu na kuwapatia hifadhi; ili hatimaye, waweze kurejeshwa tena katika maisha ya kijamii. Watu waoneshe ujasiri wa kuwafichua wale wote wanaojihusisha na biashara haramu ya binadamu na vyombo vya ulinzi, sheria na haki vitekeleze dhamana na wajibu wake pasi na makunjanzi. Inasikitisha kuona kwamba, watu wanatumia umaskini na ujinga wa watu kuwanyanyasa kwa kuwatumbukiza katika biashara haramu ya binadamu na hatimaye, kuwageuza kuwa ni vyombo vya kutosheleza tamaa zao mbovu!

Shirika la Kazi Duniani, ILO linasema kwamba, si rahisi kuweza kupata idadi kamili ya watu wanaotumbukizwa katika utumwa mamboleo. Wanawake na watoto ndio waathirika wakuu wa biashara haramu ya binadamu wanaounda walau asilimia 70% ya zaidi ya watu millioni ishirini na moja. Wengi wao ni wale wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya ngono; asilimia 40% wako katika hali ya utumwa kamili.

Takwimu zinaonesha kwamba, nchini Italia wanawake na wasichana wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu wanapelekwa kwenye biashara ya ngono. Wengi wa wanawake na wasichana hawa ni kutoka Nigeria na Ulaya ya Mashariki katika zile nchi ambazo Ukomunisti ulikuwa unashamiri kwa kiasi kikubwa. Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Caritas, linasema, kati ya wanawake wengi kutoka Nigeria wanaoomba hifadhi ya kisiasa, chini yake kuna fichama biashara haramu ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.