2016-02-06 15:57:00

Waamini wanahamasishwa kujenga na kudumisha amani duniani!


Dini zina mchango mkubwa katika kukuza na kudumisha haki na amani duniani kwa kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; kwa kutambua kwamba, huu ni msingi katika mchakato wa kukuza na kudumisha haki na amani. Waamini wa dini mbali mbali wanapaswa kutambua kwamba, wanashirikishana tunu msingi katika maisha yao; tunu ambazo zinafumbata kwa namna ya pekee, utu wa binadamu.

Haki inajikita pia katika umoja unaowataka binadamu kutambua kwamba, wao wanaunda familia ya binadamu inayosimikwa katika umoja na udugu; tayari kusimama kidete kulinda na kudumisha mafao ya wengi sanjari na matumizi sahihi ya rasilimali ya dunia, kielelezo cha neema na upendo wa Mungu kwa binadamu wote, hususan maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Haya ndiyo mawazo mazito yaliyotolewa na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani wakati akishiriki katika mkutano wa kimataifa uliokuwa unaojadili kuhusu mchango wa dini katika mchakato wa upatikanaji wa haki na amani duniani, uliofanyika Jumamosi tarehe 6 Februari 2016 huko Qom, kwenye Kituo cha Sheria cha Aemr Athar, nchini Iran. Mkutano huu umehudhuriwa na wakufunzi na wanafunzi wa masuala ya kidini.

Waamini wa dini mbali mbali duniani wanapaswa kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini, ili dunia iweze kuwa na amani, utulivu na maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Amani inaweza kukuzwa na kudumishwa duniani kwa kuzingatia kanuni msingi za maisha ya kiroho zinazofumbatwa katika Vitabu na Maandiko Matakatifu. Ufunuo wa Mungu unaogusa kwa namna ya pekee: taalimungu, binadamu, ekolojia, maadili na wajibu wa binadamu katika kutunza na kuendeleza kazi ya uumbaji.

Dini zinaweza kusaidia kudumisha haki na amani kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa upendo wa Mungu na kukombolewa na huruma yake. Kutokana na utu wao, binadamu wanaweza kushirikiana na kushikamana na kwamba, vita na machafuko ni matokeo ya binadamu kutengana na kubaguana na hatimaye, kumwacha Mwenyezi Mungu ambaye kimsingi ni chemchemi ya maisha. Katika mwelekeo wa namna hii binadamu anajichumia maafa!

Kardinali Turkson anakaza kusema, haki inajikita pia katika: umoja na mshikamano; kwa kuheshimiana, kuthamiana na kutenda kwa usawa, ili kujenga na kudumisha familia ya binadamu inayojikita katika udugu kwa kutakiana mema na ustawi; mambo yanayojikita katika mshikamano unaoongozwa na kanuni ya auni, kwa ajili ya mafao ya wengi kama kielelezo cha maisha jamii kwa ajili ya mafao ya wengi; mambo ambayo yamewekwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mahitaji ya watu wake duniani.

Kwa kuzingatia kanuni hizi, waamini wa dini mbali mbali wanaweza kuwa ni mashuhuda na vyombo vya haki na amani duniani. Kanuni hizi zinajikita katika utu wa binadamu, haki, umoja, udugu, mafao ya wengi na matumizi sahihi ya rasilimali ya dunia yanayonesha kwa namna ya ajabu upendo wa Mungu katika matendo. Wakristo anasema Kardinali Turkson wanaamini kwamba, dini zinaweza kusaidia upatikanaji wa amani duniani kwa kujikita katika mshikamano wa upendo kwa Mungu na jirani; huruma na umoja sanjari na utunzaji bora wa mazingira. Huu ni mchakato unaohitaji ushiriki wa watu wote pasi na ubaguzi. Kanuni maadili katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha haki na amani duniani.

Kardinali Peter Turkson mwishoni anasema, waamini wa dini mbali mbali hawana budi kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, kwa kulinda na kudumisha mazingira nyumba ya wote; kwa kushikamana pamoja na kuwasaidia maskini; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.