2016-02-06 15:17:00

Ratiba elekezi wakati wa hija ya Papa Francisko nchini Mexico


Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Mexico kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 18 Februari 2016 itakuwa na mwelekeo wa kiekumene ambao utamwezesha Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 12 Februari 2016 kukutana na kuzungumza na Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima, kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Josè Marì, Havana Cuba. Kwa mara ya kwanza viongozi hawa wawili wa Kanisa watazungumza kwa faragha na hatimaye, kutia sahihi tamko la pamoja, mwanzo mpya wa majadiliano ya kiekumene baina ya Makanisa haya mawili.

Wakristo wanahamasishwa kusali kwa bidii ili tukio hili liweze kuzaa matunda yanayokusudiwa. Patriaki Kirill atawasili nchini Cuba, hapo tarehe 11 Februari 2016. Hii itakuwa ni hija yake ya kwanza ya kitume kama Patriaki wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Russia nzima kutembelea Amerika ya Kusini, hususan katika nchi za Cuba, Brazil na Paraguay. Siku hii pia atawasili nchini Cuba, Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Umoja wa Wakristo.

Padre Federico Lombardi Msemaji mkuu wa Vatican anafafanua kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuondoka mjini Roma Ijumaa, tarehe 12 Februari 2016 majira ya saa 1:45 kwa saa za Ulaya. Baada ya safari ya masaa kumi na mawili na dakika kumi na tano, atawasili mjini Havana, Cuba majira ya saa 8:00 mchana kwa Saa za Cuba na Rais Raul Castro wa Cuba atampokea mgeni wake kwa heshima zote za kitaifa. Tukio hili litahudhuriwa na viongozi wa Kanisa na Serikali kutoka Cuba.

Saa 8:15 mchana kwa saa za Cuba, Baba Mtakatifu Francisko atafanya mazungumzo ya faragha na Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima na baadaye wataweka sahihi kwenye Tamko la pamoja, mwanzo mpya wa majadiliano ya kiekumene baina ya Makanisa haya mawili. Mazungumzo haya yanatarajiwa kudumu walau si chini ya saa moja na baadaye, watabadilishana zawadi, kama kumbu kumbu ya tukio hili la kihistoria. Viongozi hawa wawili pia wanatarajiwa kutoa hotuba zao ili kuonesha furaha inayobubujika kutoka kwenye visima vya huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko ataendelea na hija yake ya kitume nchini Mexico anakotarajiwa kuwasili baadaye usiku. Majimbo ambayo hayajawahi kutembelewa na Mtakatifu Yohane Paulo II na Papa Mstaafu Benedikto XVI yameingizwa katika ratiba, ili familia ya Mungu katika maeneo haya, iweze kutangaziwa na kushuhudiwa huruma ya Mungu.

Jumamosi, tarehe 13 Februari 2016, Baba Mtakatifu Francisko atatembelea Madhabahu ya Bikira Maria wa Guadalupe, Msimamizi wa Amerika ya Kusini, kitovu cha Ibada ya Baba Mtakatifu kwa Mama wa Mungu. Majira ya asubuhi, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na Rais wa Mexico, wabunge na baadaye atakutana na Baraza la Maaskofu Katoliki Mexico.

Jumapili tarehe 14 Februari 2016, Baba Mtakatifu atatembelea mji wa Ecatepec de Morelos, eneo ambao lina wakazi wengi wanaoogelea katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato! Huko Baba Mtakatifu anataka kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu kwa kutambua kwamba, maskini ndio walengwa wa Habari Njema ya Wokovu. Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na baadaye kutembelea Hospitali ya watoto, lakini kwa namna ya pekee atapita kwenye wodi za watoto wenye saratani.

Jumatatu tarehe 15 Februari 2016, Baba Mtakatifu Francisko atatembelea mji wa Tuxtla Gutierrez mji mkuu wa Chapas; kituo kikuu cha wahamiaji kutoka Guatemala. Hapa Baba Mtakatifu Francisko ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu. Hapa Baba Mtakatifu atatoa Waraka unaohamasisha mchakato wa Utamadunisho kwa kuwaruhusu waamini kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa lugha asilia. Baba Mtakatifu atapata chakula cha mchana na wenyeji wa mji huu.

Jioni atawatembelea wagonjwa na walemavu watakaokuwa wamekusanyika kwenye Kanisa kuu, mahali ambamo kuna masalia ya Askofu Bartolomè de Las Casas. Baba Mtakatifu atahitimisha siku kwa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya familia kwenye Uwanja wa michezo wa Tuxtla Gutierrez na baadaye jioni atarejea Jijini Mexico.

Jumanne tarehe 16 Februari 2016, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na Wakleri pamoja na watawa. Mchana atapata nafasi ya kuzungumza na watoto wanaohudhuria mafundisho ya katekesi. Jioni atakutana na kuzungumza na umati wa vijana wa kizazi kipya kutoka sehemu mbali mbali za Mexico.

Jumatano tarehe 17 Februari 2016, Baba Mtakatifu atatembelea eneo la Ciudad Juarez, lililoko mjini Chihuahua, Kaskazini mwa Mexico karibu na mpaka wa Marekani. Hapa Baba Mtakatifu anatarajiwa kuzungumza na wafungwa kwenye Gereza kuu la Mexico; wafanyakazi na baadaye wananchi ambao wengi wao wamekuwa ni wahanga wa vita na mashambulizi ya kigaidi.

Baba Mtakatifu Francisko ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanda unaotenganisha Mexico na Marekani, eneo ambalo ni alama ya taabu na mahangaiko ya wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta usalama na maisha bora zaidi. Hapa familia ya Mungu kutoka Marekani inatarajiwa pia kushiriki katika Ibada hii ya Misa Takatifu. Baba Mtakatifu atasimika Msalama wa Matumaini na kusali kwa ajili ya kuwaombea wale wote waliopoteza maisha yao wakiwa njiani kuelekea kwenye nchi iliyojaa maziwa na asali.

Alhamisi tarehe 18 Februari 2016, Baba Mtakatifu Francisko atakuwa anakunja vilago vya hija yake ya kumi na mbili ya kitume nchini Mexico, tayari kurejea tena mjini Vatican kuendelea na maisha na utume wake. Anatarajiwa kuwasili mjini Roma majira ya saa 9: 15 kwa saa za Ulaya.

Kama kawaida, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican itakula sahani moja nawe wakati wote wa hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Mexico, lakini ukiwa na haraka zako, zama kwenye mtandao wa Radio Vatican, hapo utavumbua siri ya urembo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.