2016-02-06 17:20:00

Mwaka wa Mahakama 2016 wazinduliwa mjini Vatican


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumamosi, tarehe 6 Februari 2016 ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kuzindua Mwaka wa 81 wa Mahakama ya mji wa Vatican. Professa Gian Piero Milano, Mhamasishaji wa amani mjini Vatican amepembua kwa kina na mapana shughuli mbali mbali za utekelezaji wa haki mintarafu maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Anasema, utekelezaji wa haki ni dhamana ambatanishi na utume wa huruma ya Mungu, ambayo kamwe haiwezi kuondoa haki, bali ni kilemba cha haki na kwamba, upendo ni kielelezo cha haki ya kweli.

Professa Milano anaendelea kufafanua kwamba, Sheria za Kanisa zinajikita katika msingi wa sheria na Amri za Mungu na kwamba, mwanasheria wa Vatican anapaswa kutambua Amri za Mungu ili kuweza kufikia ukweli, kudumisha usalama kazini na afya za wafanyakazi eneo la kazi; haki msingi, utu na heshima ya mwanadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza pamoja na kuzingatia ubora wa maeneo ya kazi, ili kweli mfanyakazi aweze kukuza utu wake. Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika sheria za Kanisa, kielelezo cha mchakato wa ushirikiano na mshikamano wa kitaifa na kimataifa unaotekelezwa na Vatican, ili kupambana kikamilifu na uhalifu wa kifedha kwa kutunga sheria inayopambana na utakatishaji wa fedha na ufadhili wa vitendo vya kigaidi. Vatican katika utekelezaji wa dhamana hii, inatekeleza utume wake katika maisha ya kiroho kwa kukazia kanuni maadili, ukweli, uwazi, uaminifu na uwajibikaji makini.

Kumekuwepo pia na mabadiliko katika usimamizi na uendeshaji wa kesi za jinai, mabadiliko ambayo yametekelezwa mapema kabisa tangu Baba Mtakatifu Francisko alipoingia madarakani. Vitendo vyote vya kibaguzi, biashara haramu ya binadamu, unyanyasaji wa watoto na utumwa mamboleo ni kinyume cha sheria za Vatican. Mambo yote haya ni sehemu ya usalama wa mji wa Vatican unaosimama kidete pia kulinda na kudumisha uhuru, haki na amani.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alianzisha mchakato wa mabadiliko katika sheria zinazohusu fedha kwa kutambua wahusika wakuu, sera na mikakati ya kupambana na utakatishaji wa fedha na ufadhili wa vitendo vya kigaidi. Hapa mkazo ni umakini, ukweli na uwazi na taarifa za kifedha, pamoja na kushirikiana na wadau mbali mbali wa kitaifa na kimataifa ili kuhakikisha kwamba, kanuni maadili, ukweli na uwazi vinazingatiwa kikamilifu, ili fedha na mali ya Kanisa visaidie katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaki ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Kumekuwepo na uhakiki wa mfumo wa fedha mjini Vatican unaotekelezwa na vyombo mbali mbali vya kimataifa kwa kushirikiana kikamilifu na Mamlaka ya fedha mjini Vatican. Marekebisho ya vyombo vya haki yameendelea kufanyika pia, ili kuhakikisha kwamba, mafao ya wengi, amani na utu wa binadamu unalindwa kikamilifu pamoja na kuendelea kushirikiana na wadau mbali mbali. Professa Milano amegusia shughuli mbali mbali zilizotekelezwa na vyombo vya sheria vya Vatican katika kipindi cha mwaka 2014- 2015 na kwamba, shughuli zote hizi zimetekelezwa kwa kwa ari na moyo mkuu, kwa kuzingatia ukweli na uwazi, weledi na ufanisi.

Vyombo vya haki na sheria vinamsadia Khalifa wa Mtakatifu Petro kutekeleza dhamana, wajibu bna utume wake kwa Kanisa la Kristo, ili kujenga na kuimarisha umoja, utume na huduma inayotolewa na Mama Kanisa kwa familia ya binadamu. Na kwa hotuba yake hii, Professa Gian Pietro Milano amezindua maadhimisho ya Mwaka wa shughuli za Mahakama mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.