2016-02-06 16:16:00

Kimbilieni kiti cha huruma ya Mungu!


Masalia ya watakatifu Padre Pio wa Pietrelcina na Leopoldo Mandic yaliwasili kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Ijumaa tarehe 5 Februari 2016 kwa maandamano makubwa ya waamini na mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Maandamano haya yalifuatiwa na Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa mapema asubuhi na Padre Nicholas Polichnowski, Mkuu wa Shirika la Utawa wa Watu wa Wafranciskani.

Alhamisi jioni tarehe 4 Februari 2016 waamini waliadhimisha masifu ya jioni sanjari na ibada ya maungamo iliyoongozwa na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya, Baraza ambalo limepewa dhamana ya kuratibu maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu na baadaye kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la San Salvatore, mahali ambapo kumehifadhiwa baadhi ya vifaa vya Ibada vilivyokuwa vinatumiwa na Padre Pio wa Pietrelcina.

Matukio yote haya yamehudhuriwa na umati mkubwa wa waamini waliokuwa ndani na nje ya Kanisa. Hili ni Kanisa ambalo pia ni mahali pa Sala kwa waamini wenye Ibada kwa Mtakatifu Padre Pio kwa Jimbo kuu la Roma. Ijumaa asubuhi tarehe 5 Februari 2016 baada ya Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa na Askofu mkuu Michele Castoro, mkurugenzi mkuu wa Utume wa Sala kwa Padre Pio, maandamano ya masalia ya watakatifu Padre Pio na Leopoldo yalianza taratibu kuelekea kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Kardinali Angelo Comastri, mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ndiye aliyepokea Masalia haya kwa kutoa historia fupi ya watakatifu hawa, iliyojikita zaidi katika toba na wongofu wa ndani; ushuhuda wa imani na hija zilizofanywa na watakatifu mbali mbali waliokita maisha yao katika  heri za mlimani; wakawaonjesha waamini huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Kitubio, waliyoiadhimisha kwa ibada na uchaji mkuu.

Kardinali Comastri anasikitika kusema kwamba, leo hii waamini wengi hawaoni sababu ya kukimbilia kiti cha huruma ya Mungu; wamesahau uzito wa dhambi unaovuruga mahusiano kati ya mwamini na Mwenyezi Mungu na kwamba, huruma na msamaha wa Mungu unamrudishia tena mwamini ile furaha ya ndani. Kanisa Katoliki limebahatika kuwa na wahudumu wa Sakramenti ya Upatanisho, waliopewa mamlaka ya kuwaondolea watu dhambi zao kwa kuwapatanisha na Mungu.

Waamini wajenge utamaduni wa kukimbilia mara kwa mara huruma na upendo wa Mungu. Kwa njia hii wataweza kuwa na ari na mwamko mpya wa kimissionari, ushuhuda uliotolewa na watakatifu hawa wawili. Waamini wawe na ujasiri wa kuomba na kutoa msamaha kwa wengine pamoja na kuendelea kuwaonjesha jirani zao matendo ya huruma, kielelezo cha imani tendaji kama alivyokuwa anakazia Mama Theresa wa Calcutta. Mahujaji waendelee kusali pia kwa ajili ya kuombea amani kati ya watu wa mataifa, amani kati ya familia na amani mioyoni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.