2016-02-05 17:24:00

Wajibu wa binadamu katika kulinda na kutunza mazingira!


Nia ya jumla ya Baba Mtakatifu Francisko kwa mwezi Februari, 2016 ili watu waweze kuwa na moyo wa utunzaji bora wa mazingira, zawadi waliyopewa bure na Mwenyezi Mungu, ili kuitumia na kuindeleza kwa kizazi cha sasa na kile kijacho. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa njia ya video anakumbusha kwamba, waamini na wasioamini wanatambua kwamba, ardhi ni urithi wa wote na matunda yake yanapaswa kuwafaidia watu wote.

Baba Mtakatifu anachukua fursa hii kuuliza swali la msingi, Je, ni kitu gani ambacho kinaendelea kujitokeza katika ulimwengu tunamoishi? Uhusiano kati ya umaskini na hali mbaya ya dunia ni changamoto inayohitaji sera mpya za uchumi na maendeleo; kwa kuwa pia na mfumo mpya wa maisha. Hapa kuna haja ya kuwa na wongofu wa kiekolojia unaowaunganisha binadamu wote, tayari kukombolewa kutoka katika utumwa wa ulazi wa kupindukia.

Baba Mtakatifu anasema anapenda kutoa ombi maalum kwa kila mtu ili kusimama kidete kulinda kazi ya uumbaji kwa sababu ardhi ni zawadi ambayo Mwenyezi Mungu amewakirimia binadamu wote ili waweze kuitumia na kutunza kwa ajili ya kizazi cha sasa na kile kijacho. Kuna haja ya kutunza mazingira nyumba ya wote anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Februari 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.