2016-02-05 15:39:00

Rais Edgar Chagwa Lungu wa Zambia akutana na Papa Francisko


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 5 Februari 2016 amekutana na kuzungumza na Rais Edgar Chagwa Lungu wa Zambia, ambaye baadaye amekutana na kuzungumza pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameandamana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Katika mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu na mgeni wake, wamegusia mahusiano mazuri kati ya Vatican na Zambia. Wameangalia kwa kina na mapana mchango wa Kanisa Katoliki katika medani za elimu, afya, ustawi na maendeleo ya wengi; hususan mapambano dhidi ya umaskini, mipasuko ya kijamii pamoja na kukoleza amani na maridhiano kati ya watu kwa njia ya utamaduni wa majadiliano. Viongozi hawa wawili pia wamegusia masuala msingi yenye mafao ya wengi, mintarafu changamoto ya wakimbizi, athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Mwishoni Baba Mtakatifu Francisko na Rais Lungu wamegusia pia masuala ya kimataifa, hususan vita inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao Barani Afrika na mchango wa Zambia katika mchakato wa kujenga na kudumisha amani kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.