2016-02-05 15:23:00

Papa Francisko kukutana na Patriaki Kirill wa Moscow tarehe 12 Feb. 2016


Vatican pamoja na Upatriaki wa Moscow kwa pamoja wanatangaza kwa furaha kubwa kwamba, kwa neema na baraka za Mwenyezi Mungu, Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima watakutana na kuzungumza tarehe 12 Februari 2016, huko Cuba, wakati Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kuelekea nchini Mexico.

Patriaki Kirill wa Moscow atakuwa nchini Cuba kwa ziara ya kitume. Viongozi hawa wawili watafanya mazungumzo kwenye Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Josè Marti mjini Havana Cuba na baadaye watatoa tamko la pamoja. Mkutano wa viongozi hawa wawili utakuwa ni daraja la majadiliano ya kiekumene na kuanza kuweka msingi muhimu sana wa mahusiano kati ya Makanisa haya mawili.

Hizi ni dalili za matumaini kwa watu wote wenye mapenzi mema. Wakristo wote wanahimizwa kusali ili kwamba, Mwenyezi Mungu aweze kubariki mkutano wa viongozi hawa wa Kanisa, ili hatimaye, uweze kuzaa matunda yanayokusudiwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.