2016-02-05 16:08:00

Mshikamano wa Papa Francisko kwa wakimbizi na wahamiaji!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa safari yake ya kikazi nchini Slovenia ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kufunga rasmi Mwaka wa Watawa Duniani, ameshiriki katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 25 tangu Slovenia ilipojipatia uhuru wake pamoja na kuzindua jengo la Ubalozi wa Vatican nchini humo.

Imekuwa ni fursa pia kwa Kardinali Parolin, kutoa salam za upendo na mshikamano kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria, Iraq na Afghanstan wanaohifadhiwa kwenye kambi ya wakimbizi huko Dobova. Kardinali Parolin anasema ameguswa na mahangaiko pamoja na mateso ya wakimbizi na wahamiaji hao.

Anawapongeza na kuwashukuru wafanyakazi wa Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki nchini Slovenia kwa huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji. Changamoto ya wakimbizi inapaswa kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu kwa kujikita kwanza kabisa katika mshikamano wa upendo; kwa kushirikiana na kufanya kazi kama wamoja, kwani huduma za peke peke hazina tija wala mashiko kwa wengi.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwasindikiza wahamiaji na wakimbizi kwa sala na sadaka zake anawahimiza Wasamaria wema kujisadaka na kujitoa kwa ajili ya kuwasaidia na kuwahumia wakimbizi, ili kuwaonjesha Uso wa Huruma ya Mungu, hususan wakati huu, Kanisa linapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Kardinali Parolin anakaza kusema, Kanisa halina majibu ya mkato kutokana na changamani ya wakimbizi na wahamiaji duniani, lakini linatoa kanuni msingi za kuzingatiwa yaani: utu na heshima ya binadamu; haki zao msingi pamoja na mshikamano wa dhati unaoongozwa na kanuni auni. Kardinali Parolin kwa njia ya Radio Katoliki Slovenia amewatumia wananchi wote salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, kutokana na ushuhuda na uwepo wao katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema nchini Slovenia kuishi kikamilifu maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kiini cha imani ya Kikristo, kwa kutubu na kumwongokea Mungu; kwa kushuhudia imani tendaji inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na kuambata upendo na huruma ya Mungu, chachu ya mabadiliko katika maisha ya watu. Chachu ya mabadiliko kutoka kwa Mwenyezi Mungu iko mikononi mwa watu dhaifu, lakini ina uwezo wa kubadili nyoyo za watu na kuandika historia mpya ya maisha.

Kardinali Parolin anawaomba waamini kuendelea kumsindikiza Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kwa njia ya sala na sadaka zao, kama kielelezo cha umoja na mshikamano katika maisha ya kiroho. Ushuhuda wa sala ni muhimu sana kama kielelezo na utambulisho wa Kikristo. Wakristo wanatakiwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya upendo na huruma ya Mungu kwa jirani zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.