2016-02-05 17:38:00

Mashuhuda wa harufu ya huruma ya Mungu na utakatifu!


Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma, Jumatano jioni tarehe 3 Februari 2016 alipokea Masalia ya Watakatifu Padre Pio wa Pietrelcina na Mtakatifu Leopoldo Mandic, mashuhuda wa huruma ya Mungu na harufu ya utakatifu wa maisha ya Kikristo, mfano bora wa kuigwa katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ili kuambata toba na wongofu wa ndani, tayari kuonja huruma ya Mungu.

Kardinali Vallini katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu anasema, waamini waliobahatika kukutana na watakatifu hawa, wanakiri kwamba, waliweza kunusa harufu ya utakatifu na huruma ya Mungu iliyokuwa inatolewa kwenye kiti cha huruma ya Mungu, yaani katika Sakramenti ya Upatanisho. Walionja uwepo endelevu wa huruma ya Kristo kwa waja wake. Waamini mbali mbali wametoa heshima kwa Masalia ya watakatifu hawa kwenye Kanisa San Lorenzo na San Salvatore yaliyoko mjini Roma. Wamesali na kufanya makesha.

Ijumaa jioni, tarehe 5 Februari 2016 kwa maandamano makubwa, masalia ya watakatifu hawa yatapelekwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kuwekwa pembeni ya Altare ya Maungamo. Kipindi chote hiki, masalia haya yanalindwa na Ndugu Wafrancisko Wakapuchini. Tarehe 6 na 7 Februari 2016, Kardinali Angelo Comastri ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa waamini watakaokuwepo Kanisani humo.

Tarehe 10 Februari, Jumatano ya Majivu, Kardinali Comastri ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya wafanyakazi wa Vatican pamoja na kuwapaka majivu, alama ya mwanzo wa kipindi cha Kwaresima, mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha ya watu.

Tarehe 11 Februari 2016 baada ya maadhimisho ya Misa Takatifu yatakayoongozwa na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Masalia ya Watakatifu hawa yatarejeshwa tena mahali pake. Ni watakatifu wanaoshuhudia kweli utakatifu unaojikita katika fadhila ya unyenyekevu na utii. Ni watakatifu wanaoendelea kushuhudia huruma ya Mungu kwa watu wenye shida na mahangaiko mbali mbali; watu wanawahamasisha waamini kumpenda Kristo wakati wa raha na shida, daima Kristo akipewa kipaumbele cha kwanza. Ni watakatifu wakiojisadaka katika kiti cha maungamo, mwaliko kwa Mapadre kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya Wakapuchini na baadaye atakutana na kuzungumza na wanachama wa vikundi vya Ibada kwa Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.