2016-02-04 15:19:00

Usiogope, wewe ni mtumishi asiye na faida!


Ndugu wapendwa, mama kanisa anatualika leo kutafakari juu ya mapenzi ya Mungu kwetu  na hitaji la Mungu toka kwetu sisi viumbe wake. Tunapata nafasi ya kuona jinsi Mungu anavyoita watu wake na kuwatuma kufanya kazi yake. Kifupi twaona kuwa Mungu anatushirikisha kazi yake.  Tunasikia katika masomo yetu ya leo juu ya wito wa Nabii Isaya, wito wa Mtume Paulo na wito wa mtakatifu Petro na wenzake. Mungu anapoita hutokea makutano kati ya Mungu na mwanadamu. Kwa hakika watu wote wameitwa ila katika Biblia tunapata kuona kuwa kati ya hao wote, wapo wachache wanaopata bahati ya pekee zaidi.  Wengi wetu tunapata tu ufahamu wa uwepo wa Mungu.  

Katika somo la kwanza twaona kuwa Mungu mfalme mkuu na mwenye enzi anajifunua sura yake na maserafi wanamwabudu huku wakifunika nyuso zao mbele ya utukufu wa Mungu. Adamu na Eva walijifunika mbele ya Mungu baada ya kutenda dhambi.  Maserafi wanafunika nyuso zao kwa vile utukufu wa Mungu ni mkuu mno. Ni sawa na kufunika dhambi zao. Kwa kaa la moto midomo ya Isaya inatakasika na anatambua na kupokea msamaha.

Katika Injili hatuoni viumbe kama ilivyo katika somo la kwanza. Kina Petro wanajishughulisha usiku kucha kuvua lakini bila mavuno. Yesu anakuja, na kwa amri yake ya kushusha nyavu, wanapata samaki wengi. Tendo hili ladhihirisha wazi uwepo wa Mungu. Petro na wenzake wanatambua uwepo wa Mungu kati yao. Petro anainama chini na kumwomba Bwana aondoke kwani yeye ni mdhambi. Kinachofuata ni kuwa Yesu anawataka kwa kazi nyingine. Yesu anamwambia Petro asiogope. Tunaona kuwa binadamu anakutana uso kwa uso na Mungu na kutumwa na hapa tunaona kama Isaya nao kina Petro wanaitika na wanatumwa.

Tunaona kuwa nabii Isaya na Petro, kama sisi sote tu wadhambi. Wanachofanya ni kukiri na kutambua uwepo wa Mungu na utukufu wake. Ili tuanze upya hatuna budi kutambua utukufu wake. Ni lazima utukufu huo uguse midomo yetu, mioyo yetu, roho zetu na maisha yetu yote. Maserafi wakiwa na kaa na moto lilochukuliwa toka altare hekaluni – Isa. 6:7, anagusa midomo yake na anasema kosa lako limeondolewa na dhambi zako kusamehewa. Isaya anatambua na kukubali msamaha. Anaitika wito. Hali hii mpya ikitokea kwetu, basi tutakuwa tayari kuyafanya mapenzi yake.

Katika Injili tunaona Petro akiambiwa usiogope – Lk. 5:10 na tangu sasa utukuwa mvuvi wa watu. Katika hali hii Petro alianguka miguuni pake Yesu na kumwomba aondoke mahali pale. Petro anamtambua Mungu na kukiri nguvu zake na ndicho kilichomfanya kuitika wito, kuacha yote na kumfuata Bwana.  Kilicho muhimu hapa ni kutambua uwepo wa aliye mtakatifu, ufahamu na utambuzi wa uwepo wa Mungu na kuupokea wito wa Mungu.

Jibu la mwanadamu mkosefu na mwenye dhambi ni kuukubali utume na kupokea msamaha wa dhambi. Tunamwona Nabii Isaya 6:8, Mungu anaposema nimtume nani, jibu la Isaya likawa mimi hapa nitume Bwana. Petro na wenzake waliacha kila kitu bila kuangalia nyuma na wakamfuata – Lk. 15:10. Sababu ya wito wao si wao wenyewe bali ni mapenzi yake Mungu. Ni neema ya Mungu. Ndiyo maana katika somo la pili, mtume Paulo anasema nimekuwa hivi kwa neema ya Mungu – 1Kor. 15:10. Na tangu hapo, yaani baada ya kupata neema hiyo ya Mungu, aliwekeza maisha yake yote kwa Bwana. Tukiwekeza na Bwana tutavuna mavuno mengi.

Tutambue kuwa hata leo bado Mungu anatuhitaji sana kama Isaya, kama kina Mtakatifu Petro na kama Mtume Paulo kutangaza habari njema ya pendo lake Mungu. Mungu anasuburi utayari wetu na ukubali wetu wa kuwa wamisionari, yaani kuwa tayari kufanya kazi yake Bwana. Watu walio tayari kama Petro kuacha yote na kufanya tu kazi ya Bwana. Tusiogope wala kuwa na mashaka. Mt. Gaspari alizoea kusema, kazi ni ya Bwana, yeye mwenyewe ataikamilisha. Tumwombe sana Mungu Mwenyezi ili katika jubilee hii ya huruma ya Mungu, huruma yake ituponye na azidi kuita watu wake kufanya kazi katika shamba lake.

Tumsifu Yesu Kristo.

Pd. R. Mrosso, C.PP.S.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.