2016-02-04 07:29:00

Papa Francisko: Mmissionari wa huruma ya Mungu na amani!


Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 12 – 18 Februari 2016 atakuwa na hija ya kitume nchini Mexico inayoongozwa na kauli mbiu “Papa Francisko mmissionari wa huruma na amani”. Hivi karibuni, Baba Mtakatifu alifanya mahojiano maalum na wakala wa habari kutoka Mexico, Notimex. Katika mahojiano haya Baba Mtakatifu anafafanua lengo la hija yake ya kitume nchini Mexico na umuhimu wa kulinda na kudumisha haki, amani na maridhiano; Ibada kwa Bikira Maria wa Guadalupe pamoja na changamoto za kijamii nchini Mexico.

Baba Mtakatifu anasema anakwenda nchini Mexico kama mmissionari wa huruma ya Mungu na mjumbe wa amani, dhamana inayowashirikisha wananchi wote wa Mexico kwani peke yake hawezi kufua dafu! Mexico ni nchi ambayo kwa bahati mbaya bado inaendelea kuogelea katika mapigano, rushwa na ufisadi; biashara haramu ya dawa za kulevya na mambo mengine yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Bikira Maria wa Guadalupe hapendi mambo haya kwa watoto wake wa Mexico.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, anakwenda nchini Mexico kama hujaji, ili kupata nafasi ya kusali pamoja na wananchi wa Mexico ili matatizo na changamoto zinazowakabili wananchi wa Mexico ziweze kupata ufumbuzi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, anakwenda Mexico ili kuwahamasisha wananchi kusimama kidete kupambana kufa na kupona dhidi ya rushwa na ufisadi; dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya na vita; anataka kuwaimarisha katika imani na matumaini kwa kujenga umoja wa kitaifa ili hatimaye, kufutilia mbali biashara haramu ya binadamu na makundi ya kihalifu yanayosambaza utamaduni hofu, wasi wasi na utamaduni wa kifo. Wananchi wanapaswa kuwa imara katika maisha yao ili kujenga amani, upendo na mshikamano wa dhati kwani vita inakumbatia utamaduni wa kifo!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, amani ni mchakato unaopaswa kufanyiwa kazi kila siku, kwa kujikita katika malezi ya watoto tangu wakiwa nyumbani; kwa kufahamiana, kupendana na kuelewana; mambo ambayo yanamwilishwa katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi; haki na mapendo. Hapa neno la msingi ni amani kati na kwa ajili ya wananchi wa Mexico. Wananchi wajenge utamaduni wa kujadiliana katika ngazi mbali mbali za maisha ya kijamii; tayari pia kuwasikiliza na kuwathamini wengine kwa kutambua kwamba, kukosa na kukoseana ni mtindo wa maisha, kusamehe na kusahau ni mwanzo wa hekima na utakatifu wa maisha.

Watu wajenge utamaduni wa kukosoana katika upendo na udugu. Majadiliano yasaidie kuleta mabadiliko, toba na wongofu wa ndani, ili kudumisha jamii inayojikita katika haki, amani, upendo na maridhiano. Wananchi wasipende maisha ya mkato kwa kumezwa na uchu wa mali na madaraka mambo ambayo yamekuwa ni chanzo kikuu cha vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Mexico. Baba Mtakatifu anaonya kwamba, fedha ni fedheha, mtu akiwa na uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka, mtu huyo atageuka kuwa mtumwa wa fedha, atakosa uhuru kamili na amani ya ndani. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaalikwa na Baba Mtakatifu kukimbilia huruma na tunza ya Bikira Maria wa Guadalupe kwa njia ya sala, ili kumwomba awaombee amani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, Mfalme wa amani kwa ajili ya familia, miji na nchi yote ya Mexico.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, ana ibada kubwa kwa Bikira Maria wa Guadalupe, anapokuwa katika shida, mashaka na mahangaiko ya moyoni, daima anakimbilia ulinzi, tunza na maombezi ya Bikira Maria ambaye amewahi kutembelea Madhabahu yake mara mbili. Kwanza, kundi la Wayesuit lilipotembelea eneo hili kwenye miaka 1970 na mara ya pili, akatembelea huko wakati wa hija ya kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II.

Baba Mtakatifu anasema, wakati mwingine hana hata neno la kusema, bali kushangaa tu mbele ya picha ya Bikira Maria wa Guadalupe kwa kutambua kwamba, huyu ni mama anayejali, anayelinda na kuwaombea watoto wake. Baba Mtakatifu kabla ya kuja Roma ili kushiriki katika mchakato wa kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro alikuwa amenuia kujenga Kanisa chini ya ulinzi na usimamizi wa Mtakatifu Juan Diego, huko Argentina. Huyu ni Mtakatifu msimamizi wa watunza maua duniani.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kupyaisha imani, matumaini na mapendo katika hija ya maisha yao ya kila siku na kwamba, hija hii inapania pamoja na mambo mengine kuwaimarisha ndugu zake katika imani, chanzo na kilele cha imani na huduma yake kama Padre. Hii ni changamoto kwa waamini kutoka kifua mbele, tayari kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, hasa wakati wa giza na mahangaiko ya watu.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, leo hii kuna watu wanakabiliwa na mmong’onyoko wa imani na tunu msingi za kimaadili na utu wema. Wakati huo huo, kuna watu wanatamani kuona imani ikatangazwa na kushuhudiwa; imani inayohamasisha ari na moyo wa kimissionari tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, ili kuwatangazia watu wa mataifa Habari Njema ya Wokovu. Imani ya Kanisa inapata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu ni imani inayowahamasisha waamini kujikita katika majadiliano ya kina na Kristo.

Imani hii inapaswa kushuhudiwa katika medani mbali mbali za maisha ya watu. Imani bila matendo anasema Baba Mtakatifu Francisko haina mafao kwa watu. Waamini wanapaswa kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, chachu ya kupyaisha maisha ya waamini bila kuwa na wasi wasi, woga wala makunyanzi!

Mwishoni, Baba Mtakatifu anasema anapenda kwenda nchini Mexico ili kuonja na kushuhudia imani ya watu wa Mungu nchini humo. Anapenda wananchi wa Mexico waweze kumkirimia kutoka katika utajiri wao wa imani, walau sehemu kidogo, kwani wao wanaye Mama Bikira Maria wa Guadalupe, hazina kubwa katika maisha yao ya kiroho. Baba Mtakatifu anataka kuitafuta hazina hii, ili iweze kuwa kweli ni urithi wake wa maisha ya kiroho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.