2016-02-04 08:27:00

Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa: shukrani na wajibu!


Kardinali Charles Maung Bo, mwakilishi wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa lililoadhimishwa Jimbo kuu la Cebu, Ufilippini na kuongozwa na kauli mbiu “Kristo ndani yenu, tumaini letu la utukufu” lilihitimishwa kwa Ibada ya Misa Takatifu. Kongamano hili limedhihirisha kwamba, Fumbo la Ekaristi Takatifu ni shule ya huduma, huruma na mapendo hususan kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ni mwaliko wa kuendeleza mchakato wa haki, amani na upatanisho.

Katika mahubiri yake, Kardinali Maung Bo amewataka waamini kuwa ni wajumbe wa Injili ya furaha inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Tamko la wajumbe wa Kongamano la Ekaristi Takatifu limekazia mambo makuu manne: Ekaristi Takatifu ni chakula cha uzima wa milele; ni chakula cha maskini; ni mkate wa majadiliano na ni masurufu ya utume wa Kanisa.

Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa litaadhimishwa kunako mwaka 2020 katika Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, Hungaria. Kardinali Peter Erdo’ anasema, wajumbe walioshiriki katika maadhimisho ya Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa Jimbo kuu la Cebu, kutoka nchini Hungaria wamepokea dhamana hii kwa furaha na shukrani kubwa kwa Baba Mtakatifu Francisko na kwamba, kwa njia ya mjumbe wake, wamewasilisha salam na shukrani kwa Baba Mtakatifu. Kwa mara ya kwanza, Hungaria ilikuwa mwenyeji wa Kongamano la Ekaristi Takatifu kunako mwaka 1938.

Kardinali Erdo anakaza kusema maadhimisho ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa yanaanza kuwa na mwelekeo mpana zaidi kwa kugusa uhalisia wa maisha ya watu ili kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ekaristi Takatifu ni chachu ya kukuza na kudumisha umoja, udugu na mshikamano kati ya waamini, kwa kuwa na jicho la upendo kwa walemavu ndani ya jamii. Ekaristi Takatifu ni chachu makini ya Injili ya familia inayokumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Ekaristi Takatifu, inalisukuma Kanisa kutembea bega kwa bega na vijana wa kizazi kipya kwa njia ya utume wa vijana, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Kongamano hili limewawezesha waamini kutambua umuhimu wa kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kitamaduni ili kukoleza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Kumbe, maadhimisho ya Makongamano la Ekaristi Takatifu katika ngazi mbali mbali ni fursa makini inayopania kupyaisha imani inayomwilishwa katika maisha ya watu, kielelezo makini cha imani tendaji kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu

Kardinali Erdo anasema, dhamana hii itaanza kufanyiwa kazi mapema iwezekanvyo kwa kuunda Kamati ya maandalizi ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa huko Budapest, Hungaria. Wanataka kuanza kuangalia ujumbe wa kitaalimungu na Kibiblia utakaokuwa ni kauli mbiu ya maadhimisho haya. Mambo mengine ya kuzingatia ni sanaa na muziki mtakatifu. Hii itakuwa ni chachu ya mabadiliko na upyaisho wa Liturujia nchini Hungaria. Maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi nchini Hungaria, miaka 70 iliyopita yaliacha alama ya kudumu kwa familia ya Mungu nchini humo. Hapa mwaliko kwa waamini ilikuwa ni kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kwani maadhimisho haya yalifanyika mara tu baada ya vita.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.