2016-02-03 11:16:00

Watawa endeleeni kutukuza utakatifu na ukuu wa maisha ya kitawa!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Sherehe ya Bwana Kutolewa Hekaluni, Siku ya 20 ya Watawa Duniani sanjari na kufunga Mwaka wa Watawa Duniani, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumanne jioni tarehe 2 Februari 2016 alitoka nje ya Kanisa kuu ili kukutana na kuwasalimia maelfu ya watawa waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro ili kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu hata kama hawakupata bahati ya kuingia ndani.

Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza kwa moyo wa dhati na kutumainia kwamba, ingawa hawakupata nafasi ya kuingia Kanisani, walau wameweza kushiriki Ekaristi Takatifu. Amewashukuru kwa kufunga Mwaka wa Watawa kwa pamoja na kuwataka sasa kujifunga kibwebwe kusonga mbele kwa imani na matumaini, kwa kutambua kwamba, kila mtawa anayo nafasi ya pekee na kazi maalum katika maisha na utume wa Kanisa. Daima watawa wawe na kumbu kumbu ya wito ule wa kwanza, ili kuonja tena na tena ule upendo ambao Mwenyezi Mungu anaendelea kuwaitia.

Baba Mtakatifu anawataka watawa waendelee kuutukuza uzuri na utakatifu wa maisha ya wito wao wa kwanza pamoja na kuendelea kuchakarika katika maisha na utume wa Kanisa, daima sala na tafakari ya Neno la Mungu vikipewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa watawa. Sala ni nguzo imara katika maisha ya kitawa na itawasaidia kuzeeka wakiwa na divai mpya katika maisha yao.

Baba Mtakatifu anawapongeza na kuwashukuru watawa wazee, ambao bado ndani mwao wanaendelea kuwa kweli ni mashuhuda wa moto wa furaha, imani na matumaini. Baba Mtakatifu anawataka watawa hawa kamwe wasizimishe moto wa utume wawe na moyo na ujasiri wa kusonga mbele kwa matumaini, huku wakimwomba Bwana wa mavuno ili aweze kupeleka watenda kazi wema na watakatifu katika shamba lake, ili wao pia waweze kupandikiza Injili ya furaha kwa ari na moyo mkuu.

Watawa watunze ndani mwao kumbu kumbu ya wito wao wa kwanza, daima wawe ni watu wa matumaini, ili kuwarithisha tunu bora za maisha ya Kiinjili vijana wa kizazi kipya wanaotaka kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake! Mwishoni, Baba Mtakatifu aliwaomba watawa na waamini waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kusali ili kukimbilia tunza na ulinzi wa Bikira Maria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.