2016-02-03 14:36:00

Iweni na matumaini ili kuambata huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Ecuador, mwezi Julai, 2015 iliamsha kwa namna ya pekee katika mioyo na maisha ya wananchi wengi ile ari na moyo wa kutaka kukumbatia huruma ya Mungu katika maisha yao pamoja na kumwilisha imani katika matendo ya huruma kwa maskini bila kusahau majadiliano yanayojikita katika misingi ya ukweli na uwazi, ili kupata suluhu ya kudumu katika masuala ya kisiasa na kijamii nchini Ecuador. Wananchi wanapaswa kufahamu ukweli juu ya mwenendo wa uchumi, tayari kushiriki katika maboresho yake kwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.

Haya ni kati ya mambo yaliyojadiliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Ecuador katika mkutano wake uliofanyika hivi karibuni, ili kupembua kwa kina na mapana mafanikio na changamoto zilizotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini humo. Maaskofu katika taarifa yao ya mwisho, wanapenda kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwatembelea na kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo. Hija hii imewajengea umoja na udugu, mambo msingi katika ushuhuda na mchakato wa kuimarisha imani tendaji inayojikita katika huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ecuador limekazia umuhimu wa Kanisa kuwekeza katika sekta ya kilimo ili kusaidia wananchi kuwa na uhakika wa usalama wa chakula; ufugaji bora, ili kuweza kuwaongezea wananchi kipato, ili kukabiliana na hali ngumu ya maisha pamoja na viwanda, kazi inayopaswa kufanywa na Serikali pamoja na wadau mbali mbali. Lengo ni kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi pamoja na kuwapatia wananchi fursa za ajira na uhakika wa kuwa na maisha bora zaidi. Hii ni changamoto ya kuambata mafao ya wengi badala ya kukumbatia mambo ya kisiasa yanayoongozwa na vyama vya upinzani kwa ajili ya mafao binafsi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ecuador linawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanaufanyia kazi ujumbe walioachiwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini mwao, kwa kuimarisha imani, matumaini na mapendo. Ni wakati wa kujikita katika tunu bora za maisha ya familia, Kanisa dogo la nyumbani; shule ya utakatifu haki na amani; mahali pa kupenda na kupendwa; kusamehe na kusamehewa. Wananchi wajibidishe katika kuendeleza misingi bora ya kijamii kwa kuambata mshikamano wa dhati unaoongozwa na kanuni auni na sadaka makini.

Baraza la Maaskofu katoliki Ecuador limepitisha sera na mikakati mbali mbali ya shughuli za kichungaji kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, uliozinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 8 Desemba 2015 kwa kufungua lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Waamini wanahamasishwa kuwa na matumaini wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kwa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani; tayari kufanya toba na wongofu wa ndani.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ecuador limepata kusikiliza shuhuda zilizotolewa na Mababa waliokuwa wanahudhuria Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia iliyohitimishwa hivi karibuni hapa mjini Vatican. Lengo ni kuendelea kujipanga vyema katika utume wa familia, ili kweli familia ziweze kuwa ni mdau mkubwa katika mchakato wa Uinjilishaji kwa kuambata Injili ya familia pamoja na Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Waamini wanahamaishwa kuimarisha maisha ya kifamilia kama sehemu ya kuyatakatifuza malimwengu kwa chachu ya Injili na ushuhuda wa imani tendaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.