2016-02-03 10:47:00

Hakuna sababu msingi za kuogopa China!


Baba Mtakatifu Francisko anasema kutoka moyoni mwake kwamba, anavutiwa sana na China kutokana na utamaduni na hekima yao na anamtakia heri na baraka Rais Xi Jinping wa China pamoja na watu wake wanapoadhimisha Mwaka Mpya hapo tarehe 8 Februari 2016. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, China itaendelea kusaidia na kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa katika kutunza mazingira nyumba ya wote!

Hii ni sehemu ya mahojiano ya kina kati ya Baba Mtakatifu Francisko na mwandishi wa habari Bwana Francesco Sisci yaliyochapishwa tarehe 2 Februari 2016 kwenye Gazeti la “Asia Times”.

Kutokana na umuhimu wa China katika medani mbali mbali za kimataifa kama alivyowahi kusema Matteo Ricci, Mmissionari mahiri nchini China kwamba, kuna haja ya kufanya majadiliano ya kina na China kwani imebarikiwa kuwa na utajiri mkubwa na rasilimali nyingi zinazoweza kutumika kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Kuna watu mashuhuri kama Marco Polo waliofaulu kuweza kuiga mambo kutoka China na kuyaleta Italia, leo hii umekuwa ni utajiri wa Italia.

Baba Mtakatifu anakumbuka kwa heshima na tahadhima hija yake ya kichungaji Sri Lanka na Ufilippini, aliyoitekeleza Januari 2015 kwa kukazia umuhimu wa kuendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi ili kushinda kishawishi cha woga na wasi wasi usiokuwa na mashiko, ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Ikumbukwe kwamba, amani ni kati ya changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa ikitaka, amani inaweza kutawala na kushamiri duniani.

Lengo hili linaweza kufikiwa anakaza kusema Baba Mtakatifu kwa njia ya majadiliano na hapa hakuna njia ya mkato. Majadiliano ni safari ya pamoja inayowakutanisha watu ili kwa pamoja waweze kujikita katika ustawi na mafao ya wengi kwa kuzingatia utu wa binadamu na tamaduni za watu wa mataifa, ili mambo yote haya yaweze kutumika katika kutafuta na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano.

Baba Mtakatifu akizugusia kuhusu dhana ya watoto nchini China anasema, kuna baadhi ya jamii ambazo hazina ukarimu wa kutaka kuzaa watoto na kwamba, anawashukuru na kuwapongeza viongozi wa China ambao wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu wamelegeza masharti na kwamba, wananchi wa china wanaweza kupata mtoto walau zaidi ya mmoja. Baba Mtakatifu anawataka wananchi wa China kujipatanisha na historia, mafanikio na changamoto wanazokabiliana nazo ili kupata ukomavu na ukuaji katika medani mbali mbali za maisha. Kwa njia hii pia, wananchi wa China wanaweza kujisamehe na kuanza kuangua tena kicheko, tayari kusonga mbele kwa imani na matumaini.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kutambua na kuthamini mchango wa China katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu, hususan katika tamaduni na wala hapa anasema hazungumzii masuala ya kisiasa. Wananchi wawe na ujasiri wa kukabiliana na changamoto za kiuchumi ili kuleta maboresho makubwa yanayotarajiwa na wengi, kwa kuwa na matumaini yaliyo bora zaidi pasi na kukata tamaa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.